Hai Dc yajifunza mbinu za kuongeza mapato Jiji la Dodoma
Na. Coletha Charles, DODOMA
Halmashauri
ya Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro imefanya ziara katika Halmashauri ya Jiji
la Dodoma kujifunza mikakati ya kuongeza mapato ya ndani na kuboresha mifumo ya
ukusanyaji.
Akizungumza
wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Edmund
Rutaraka alisema kuwa wamefika Halmashauri ya Jiji la Dodoma kupata uzoefu wa
mikakati inayotumika kuongeza mapato.
Alisema
kuwa mapato ya ndani ni muhimu katika kuiwezesha halmashauri kujiendesha kwa
ufanisi, kutekeleza majukumu yake na kuendelea kutoa huduma muhimu kwa
wananchi.
“Lengo
kubwa la sisi kuja hapa ni kuona namna gani mnavyoweza kukusanya mapato yenu,
na sisi tuweze kuona tutachukua hizo mbinu kama zitafaa kwenye halmashauri
yetu, basi tuweze kukusanya zaidi,” alisema Rutaraka.
Kwa
upande wake, Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Bakari Fundikira
alisema kuwa jiji hilo limeweka mikakati mbalimbali ya kuboresha ukusanyaji wa
mapato kwa kuanzisha kanda.
Alisema
kuwa uzoefu wa jiji hilo katika ukusanyaji wa mapato utawasaidia viongozi na
wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai kubaini mbinu zinazoweza kutumika
kuongeza mapato katika halmashauri yao.
“Zile
kanda zimesogeza baadhi ya huduma karibu na wananchi, jambo ambalo limeturahisishia
ukusanyaji na kufanya mchakato huo kuwa rahisi zaidi,” alisema Fundikira.
Nae,
Afisa Mapato wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Jackson Magawa alisema kuwa jiji
hilo limegawanya maeneo yake katika kanda saba za huduma kulingana na shughuli
za kiuchumi, hali inayorahisisha ukusanyaji wa mapato.
Alisema
kuwa kanda ya kwanza ina maeneo yenye maduka mengi pamoja na soko la
wafanyabiashara wadogo, huku kanda ya pili ikiwa na maeneo ya kibiashara
yanayozalisha mapato kupitia ardhi.
“Kanda
ya tatu ni maeneo ya viwanda, ambako tunapata mapato kwa kiasi kikubwa kupitia ‘service
levy’. Kanda ya nne ni maeneo ya makazi Dodoma Makulu, Kanda ya tano ni maeneo
ya pembezoni Kikuyu, Kanda ya sita ni maeneo ya pembezoni Mipango na Kanda ya saba
ni maeneo ya pembezoni huko Hombolo,” alisema Magawa.
Ziara
hiyo imejumuisha viongozi na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai,
wakiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, waliotembelea Halmashauri ya
Jiji la Dodoma kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu mikakati ya kuongeza
mapato ya ndani.
MWISHO
Comments
Post a Comment