Jamii yatakiwa kuimarisha ulinzi wa watoto dhidi ya ukatili Dodoma
Na. Coletha Charles, MNADANI
Wazazi na walezi wametakiwa kuimarisha usimamizi na
malezi ya watoto ili kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kingono, unyanyasaji
na changamoto za afya ya akili zinazohatarisha ustawi wa watoto katika jamii.
Wito huo umetolewa na Afisa Ustawi wa Jamii, Aneth Mwambya wakati wa maadhimisho ya SALiKi na Samia Day 2026, yaliyofanyika katika Shule ya Msingi Jitegemee, Kata ya Mnanda, Jiji la Dodoma.
Alisema kuwa malezi ya watoto ni jukumu la pamoja
linalopaswa kuanzia katika familia, akibainisha kuwa shughuli za kutafuta
maendeleo ya kiuchumi hazipaswi kuwafanya wazazi kupuuza usalama na mahitaji ya
watoto wao.
“Malezi yanaanzia kwenye familia, wazazi tunapaswa
kuzungumza na watoto, kuwapa mapenzi ya dhati, kuwafundisha maadili mema na
kufuatilia mienendo yao badala ya kutegemea adhabu kali kila wanapokosea,”
alisema Mwambya.
Aidha, aliongeza kuwa baadhi ya watoto wanakabiliwa na ukatili unaodaiwa kufanywa na watu wa karibu, wakiwamo ndugu na watu wanaoaminika, hali inayohitaji wazazi kuongeza uangalizi na kuchukua hatua wanapobaini viashiria vya hatari.
Kwa upande wake, mkazi wa Mtaa Mbwanga, Joyce John
alisema kuwa ujumbe uliotolewa umeonesha umuhimu wa jamii kushiriki kikamilifu
katika malezi na ulinzi wa watoto, badala ya kusubiri mamlaka za serikali
zichukue hatua pekee.
Alisema kuwa wazazi wanapaswa kuwa karibu na watoto
wao, kufuatilia mienendo yao na kutoa taarifa kwa mamlaka husika wanapobaini
viashiria vya ukatili ili kuhakikisha watoto wanakua katika mazingira salama.
“Wazazi na walezi tunapaswa kuweka kipaumbele katika
malezi bora, kwani ushirikiano wa familia na jamii ni msingi wa kuzuia ukatili
na kulinda mustakabali wa watoto,” alisema John.
Kwa ujumla, jamii imetakiwa kushirikiana katika malezi
na ulinzi wa watoto, kutoa taarifa za ukatili kupitia namba 116 na kuhakikisha
manusura wanapata huduma kwa wakati, huku vituo vya afya vikitumika kutoa
msaada wa kitabibu, kisaikolojia na kisheria kwa waathirika wa ukatili.


Comments
Post a Comment