Hai DC yajifunza kuimarisha usafi na usimamizi wa taka Jiji la Dodoma

Na. Mwandishi wetu, DODOMA

 

Viongozi na wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro wamejifunza mbinu za usafi wa mazingira na usimamizi wa taka katika Jiji la Dodoma kwa lengo la kuboresha usafi na kuimarisha utunzaji wa mazingira.

 


Ziara hiyo ilijumuisha kutembelea Dampo la Chidaya lililopo Jiji la Dodoma, ambako wajumbe walijifunza taratibu za upokeaji, utenganishaji, usafirishaji na uhifadhi wa taka.

 

Afisa Uendeshaji wa Dampo, Elias Banyikila alisema kuwa Dodoma huzalisha wastani wa tani 594 za taka kwa siku, huku tani 392 zikipokelewa d

Dampo la Chidaya na tani 54 zikirejele­zwa.

 

Alisema kuwa dampo hilo lina ukubwa wa ekari 48, lakini takribani ekari 12 pekee ndizo zinazotumika, likiwa na miundombinu inayojumuisha uzio, ofisi, mizani, nyumba za walinzi na mitambo.

 


“Dampo hili linapokea taka za kawaida kutoka majumbani na masokoni, lakini taka hatarishi, ikiwemo za hospitalini, hushughulikiwa kwa utaratibu maalumu,” alisema Banyikila.

 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Edmund Rutaraka alisema kuwa ziara ya kujifunza usimamizi wa taka katika Jiji la Dodoma itasaidia halmashauri hiyo kuandaa dampo la kisasa litakalokidhi mahitaji ya wananchi.

 

Alisema kuwa wamejifunza namna ya kuendesha dampo na kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza, ili kuhakikisha uwekezaji huo unakuwa endelevu na kulinda mazingira.

 

“Tupo kwenye utaratibu wa kutafuta eneo la dampo. Ziara hii imetusaidia kujifunza mchakato mzima ili tuweze kujenga dampo la kisasa litakalokidhi mahitaji ya wananchi wetu,” alisema Rutaraka.

 

Nae, Afisa Mazingira wa Kitengo cha Usafi na Udhibiti wa Taka, Rose Makinda alisema kuwa huduma za usafi Dodoma hutolewa kwa ushirikiano wa kampuni na vikundi, vinavyoshiriki ukusanyaji, usafirishaji na urejelezaji wa taka.

 


“Shughuli za usafi na usimamizi wa taka zinaongozwa na sheria mbalimbali, ikiwemo Sheria ya Afya ya Jamii ya mwaka 2009 na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, pamoja na sheria za Jiji la Dodoma za mwaka 2022,” alisema Makinda.

 

Ziara hiyo imeweka msingi wa Halmashauri ya Hai kutathmini mbinu zinazoweza kutekelezeka katika mazingira yake, kwa lengo la kuimarisha usafi, kupunguza athari za taka na kukuza fursa za urejelezaji.

 

MWISHO

Comments

Popular Posts

Kata ya Matumbulu wanufaika na Mil. 114.7 Maadhimisho ya Samia Day

Samia Day 2026 yaibua vipaji vya michezo Kata ya Matumbulu