Wananchi Dodoma watakiwa kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote

Na. Coletha Charles, MAJENGO

 

Mkoa wa Dodoma umezindua rasmi awamu ya pili ya Bima ya Afya kwa Wote, ukilenga kuongeza upatikanaji wa huduma za matibabu na kupunguza gharama zinazobebwa na wananchi wanapougua.

 


Akizungumza katika uzinduzi uliofanyika katika Soko la Wazi la Machinga, Kata ya Majengo, jijini Dodoma Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri alisema kuwa ushirikiano wa viongozi na wananchi ni muhimu kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kwa mafanikio.

 

Alisema kuwa bima ya afya ni njia muhimu ya kulinda familia dhidi ya gharama za matibabu, akiwataka wananchi kujiunga mapema ili kupata huduma wanapozihitaji badala ya kusubiri kukabiliwa na changamoto za kiafya.

 

“Kila mmoja wetu ana jukumu la kuhakikisha hakuna mwananchi anayeachwa nyuma katika jitihada hizi za bima ya afya. Ugonjwa unaweza kumpata mtu yeyote wakati wowote, sasa fursa hii itumie vizuri,” alisema Alhaj Shekimweri.

 

Aidha, alizitaka halmashauri kufuatilia uandikishaji, upatikanaji wa dawa na ubora wa huduma, huku taarifa zikitumika kutatua changamoto. “Hatupaswi kutoa taarifa kwa lengo la kufurahisha viongozi. Tunapaswa kutoa taarifa za kweli zitakazotuwezesha kubaini mapungufu na kupata utatuzi,” alisema Alhaj Shekimweri.

 

Kwa upande wake, Meneja wa Mkoa wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Irene Kataraihya alisema kuwa huduma za bima zimeendelea kuwafikia watumishi, wafanyabiashara na makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mifumo na vifurushi vinavyotolewa.

 


Alisema kuwa wanachama wanapata huduma katika vituo mbalimbali, kuanzia zahanati na vituo vya afya hadi hospitali za wilaya, mkoa na rufaa, zikiwemo Hospitali ya Benjamin Mkapa na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kwa kuzingatia taratibu husika.

 

Uzinduzi huo unatarajiwa kuongeza mwamko wa wananchi kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote, huku mafanikio ya mpango huo yakitegemea ushirikiano wa serikali, NHIF na jamii katika kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za matibabu bila kuzuiwa na gharama, hatua inayolenga kulinda afya na ustawi wa familia za Watanzania.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Vikundi vya Kata ya Kizota vyapatiwa elimu ya mikopo ya 10%

JIJI LA DODOMA LAJA NA TEKNOLOJIA YA NISHATI MBADALA MAONESHO YA NANENANE

Wananchi watakiwa kuunga mkono juhudi za usafi wa Mazingira