NHIF yaachana na utaratibu wa kusubiri wananchi ofisini

Na. Mwandishi Wetu, DODOMA

 

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) wapongezwa kwa hatua ya kuwafuata wananchi katika maeneo yao ili kuwapatia elimu na huduma za afya, badala ya kusubiri wananchi wafike katika ofisi.

 


Hayo aliyasema Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabiri Shekimweri wakati wa uzinduzi wa Bima ya Afya kwa Wote Awamu ya Pili, Mkoa wa Dodoma, uliofanyika katika Soko la Wazi la Machinga.

 

Alisema kuwa eneo hilo ni muhimu kwa kuwa linakutanisha makundi mbalimbali ya wananchi, wakiwemo wafanyabiashara, madereva na wananchi kwa ujumla.

 

“Niwapongeze NHIF kwa kuchagua eneo hili la Machinga, ambalo lina wananchi wa makundi mbalimbali. Niwaombe muendelee na utaratibu huu wa kuwafuata wananchi katika maeneo yao badala ya kukaa ofisini na kuwasubiri. Hii itasaidia wananchi wengi zaidi kufikiwa na kupata huduma” alisema Alhaj Shekimweri.

 

Aliongeza kuwa hatua hiyo inaonesha umuhimu wa kusogeza huduma karibu na wananchi, hususan wale ambao shughuli zao za kila siku zinaweza kuwapa changamoto ya kufika katika ofisi za huduma.

 


Kwa upande wake, mwananchi wa Kata ya Kizota, Ibrahim Hussein aliishukuru NHIF kwa kusogeza huduma za afya karibu na wananchi, akieleza kuwa huduma hizo haziishii katika upatikanaji wa bima pekee, bali pia zinajumuisha upimaji wa magonjwa mbalimbali na utoaji wa ushauri wa afya.

 

“Awali ya yote, tunashukuru kwa huduma mnazoendelea kutupatia katika maeneo yetu. Mbali na kupata elimu kuhusu bima ya afya, tunapata pia fursa ya kupima magonjwa mbalimbali na kupata ushauri wa afya. Tunawashukuru sana kwa kutufikia katika maeneo yetu” alisema Hussein.

 

Uzinduzi huo ni sehemu ya juhudi za kusogeza huduma za bima ya afya karibu na wananchi, kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kuwa na bima ya afya na kuhamasisha makundi mbalimbali kushiriki katika mfumo wa huduma za afya.

Comments

Popular Posts

Vikundi vya Kata ya Kizota vyapatiwa elimu ya mikopo ya 10%

JIJI LA DODOMA LAJA NA TEKNOLOJIA YA NISHATI MBADALA MAONESHO YA NANENANE

Wananchi watakiwa kuunga mkono juhudi za usafi wa Mazingira