Dodoma English Medium kusomesha kwa gharama nafuu

 

Na. Mwandishi wetu,

MRADI wa ujenzi wa Shule ya Awali na Msingi Dodoma English Medium umewasaidia wazazi wenye kipato cha kati kusomesha watoto wao katika shule ya mchepuo wa kiingereza karibu na maeneo yao kwa gharama nafuu.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prisca Myalla alipokuwa akisoma taarifa ya mradi wa ujenzi wa Shule ya Awali na Msingi ya Dodoma English Medium kwa Kiogozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2024.

Akiongelea faida za mradi huo alizitaja kuwa ni kuwasaidia wazazi wenye kipato cha kati kupata fursa ya kusomesha watoto kwenye shule ya mchepuo wa kiingereza. Faida nyingine aliitaja kuwa ni wananchi kusogezewa huduma ya shule karibu ambapo watoto walikuwa wanasafiri umbali mrefu kufuata huduma ya elimu pia wanafunzi wanapata elimu bora kwa gharama nafuu ukilinganisha na shule binafsi. “Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024, mradi umelenga kutoa elimu bora ambayo itasaidia kupata wataalamu mbalimbali kwa maendeleo ya uchumi kwa Taifa letu, kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, kuongeza uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la awali na msingi na kuwezesha wananchi wenye kipato cha kati kuwapeleka watoto katika shule za mchepuo wa kiingereza” alisema Myalla.

Akiongelea gharama za mradi alisema kuwa utekelezaji wa mradi huo ulianza tarehe 05 Mei, 2023 na kukamilika tarehe 30 Desemba, 2023 kwa gharama ya shilingi 458,047,800.00. Ndugu Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024, shule hii iliwekewa jiwe la msingi na Abdalla Shaib Kaimu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023 tarehe 03 Oktoba, 2023. Pia tunatoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuendelea kuboresha sekta ya elimu kwa kuimarisha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia. Halmashauri ya Jiji la Dodoma inaahidi kutunza miundombinu ya shule hii” alisema Myalla.

Shule ya Awali na Msingi Dodoma English Medium yenye usajili namba EM 20048, ipo Kata ya Ipagala, Mtaa wa Swaswa yenye ukubwa wa eneo la mita za mraba 35,400 ikiwa na jumla ya wanafunzi 270 wavulana 147 na wasichana 123 na walimu 14. Shule inatekeleza jumbe za Mwenge wa Uhuru 2024 kwa vitendo, kupitia ujumbe wa “Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa ujenzi wa Taifa endelevu” ambapo shule imepanda miti 446 kati ya hiyo miti 279 ni ya matunda na miti 167 kwa ajili ya kivuli.

MWISHO

 

Comments

Popular Posts

Wananchi Makutupora wafunguka changamoto ya Maji, Umeme na Shule kwa Mkuu wa Mkoa

Waziri Mchengerwa apongeza usimamizi wa miradi jijini Dodoma

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma