Vijana watakiwa kujiendeleza nje ya mfumo rasmi
Na. Lulu Luvanda, DODOMA
Jamii imetakuwa kuwahamasisha vijana waliokosa elimu
katika mfumo rasmi kujiunga na Mpango wa Elimu Changamani kwa Vijana walio nje
ya shule nchini Tanzania (IPOSA) ili kupata fursa ya kujiendeleza kielimu nje
ya mfumo rasmi.
Akizungumza katika maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu wazima na nje ya mfumo rasmi yanayofanyika katika viwanja vya Nyerere square, Afisa Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi wa Elimu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Annamaria Kidunda, alisema kuwa IPOSA inalenga kuwapa fursa vijana na wanafunzi ambao walishindwa kuendelea na mfumo rasmi wa elimu kupata nafasi nyingine ya kupata elimu nje ya mfumo rasmi.
Kwa mujibu wa Kidunda, IPOSA ni darasa linalowahusisha
wanafunzi waliokatisha masomo au kushindwa kuendelea na mfumo rasmi wa elimu,
kwa kuwawezesha kupata elimu na mafunzo yatakayowasaidia kukabiliana na
mahitaji ya maisha ya sasa.
Alisema kuwa programu hiyo inalenga kuondoa pengo katika
elimu kwa kuwapatia walengwa maarifa na stadi mbalimbali zitakazowawezesha
kujitegemea, kuboresha maisha yao na kushiriki katika shughuli za maendeleo ya
jamii. Mpango huo pia unatekelezwa kwa udhamini wa wadau wa UNICEF na Serikali
ya Canada.
Kwa upande wa mnufaika ambae ni mwanafunzi wa IPOSA
kutoka Wilaya ya Chamwino, Baraka Elias alisema kuwa elimu hiyo imemsaidia
kupata maarifa ambayo amekuwa akiyatumia katika kuelimisha na kuielekeza jamii
yake kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira.
Alisema kuwa kupitia elimu aliyopata katika IPOSA,
ameweza kuelewa kwa kina nafasi ya mtu binafsi katika kutunza mazingira na
kuhamasisha jamii kuchukua hatua za kulinda mazingira kwa manufaa ya kizazi cha
sasa na kijacho.
Nae mwanafunzi na mnufaika wa IPOSA, Vestina Tumbi alisema
kuwa mpango huo umemjengea uwezo wa kujitegemea kiuchumi baada ya kupata
maarifa na ujuzi ambao umemsaidia kuanzisha na kuendesha biashara zake.
Maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima
yanaendelea kutoa nafasi kwa wananchi na wadau mbalimbali kuelewa namna elimu
nje ya mfumo rasmi inavyoweza kuwa daraja la kuwafikia vijana na watu ambao
wamekosa fursa ya kuendelea na elimu katika mfumo wa kawaida yakiongozwa na
kaulimbiu isemayo “Kisomo kwa
Manufaa ya Watu, Dunia na Ustawi wa Jamii,”.
Comments
Post a Comment