Elimu changamani yawawezesha vijana walio nje ya mfumo rasmi wa elimu
Na. Amoni Sambulila, DODOMA
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino kupitia mpango wa
Elimu Changamani kwa Vijana Walio Nje ya Mfumo Rasmi wa Elimu (IPOSA)
inaendelea kuwawezesha vijana waliokumbwa na changamoto mbalimbali na kushindwa
kuendelea na masomo katika mfumo rasmi wa elimu, kwa kuwapatia elimu, ujuzi wa
ujasiriamali na ufundi stadi.
Akizungumza kuhusu mpango huo, Afisa Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi, wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Annamaria Kidunda alisema kuwa IPOSA huwapa vijana walio nje ya mfumo rasmi wa Elimu fursa ya kupata ujuzi wa ujasiriamali na ufundi stadi, ikiwemo ushonaji wa nguo, unaowasaidia kujitegemea na kukabiliana na changamoto za maisha.
Alisema hayo leo, Jumanne, tarehe 18 Agosti, 2026
katika muendelezo wa maadhimisho ya Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo
Rasmi, yanayofanyika Nyerere Square, Jijini Dodoma.
Kwa upande wake Maria Jofrey, mmoja wa wanufaika wa IPOSA,
alisema kuwa mpango huo umemsaidia kupata ujuzi mbalimbali wa ujasiriamali,
ikiwemo kutengeneza ubuyu, sabuni na tambi, pamoja na mafunzo ya ufundi stadi
ya kushona nguo.
Nae Ketina Jumanne, mnufaika wa IPOSA, alisema kuwa
mpango huo umekuwa chachu kwa vijana waliokosa fursa ya kuendelea na masomo
kutokana na changamoto mbalimbali, ikiwemo kufeli, ujauzito na magonjwa, kwa
kuwapa nafasi ya kuendelea kujifunza na kupata ujuzi unaowawezesha kujitegemea.
Kupitia IPOSA, Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
inaendelea kutoa fursa kwa vijana walio nje ya mfumo rasmi wa elimu kupata
elimu na ujuzi wa ujasiriamali na ufundi stadi, kwa lengo la kuwawezesha
kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya jamii.
Comments
Post a Comment