Chuo Kikuu Huria chaungamkono kaulimbiu ya Kisomo kwa manufaa ya jamii
Na. Rahma Magona, DODOMA
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kimeeleza namna
kinavyotekeleza kaulimbiu ya Maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima na
Elimu Nje ya Mfumo Rasmi kupitia programu mbalimbali zinazolenga kuwapatia
wanafunzi maarifa na ujuzi wenye manufaa kwa watu, dunia na ustawi wa jamii.
Maelezo hayo yalitolewa leo tarehe 18 Agosti, 2026 katika maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi yanayofanyika katika Viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma.
Akizungumza katika banda la Chuo Kikuu Huria cha
Tanzania, Afisa Udahili wa Chuo Kikuu Huria Tawi la Dodoma, Eliud Asajile alisema
kuwa chuo hicho kinakwenda sambamba na kaulimbiu ya maadhimisho hayo kupitia
programu zinazolenga kuandaa wanafunzi wenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya
jamii. “Tuna programu kama ‘Certificate in Social Work’ inayotekeleza kaulimbiu
ya ‘Kisomo kwa Manufaa ya Watu, Dunia na Ustawi wa Jamii’, kwa kumpa mwanafunzi
maarifa ya kuwasiliana na jamii, kutambua mahitaji yake na kusaidia kuyafikia,”
alisema Asajile.
Aliongeza kuwa kupitia programu hiyo, wanafunzi
wanajengewa uwezo wa kutumia elimu wanayoipata katika kuisaidia jamii kwa
kutambua changamoto na mahitaji yake na kushiriki katika kutafuta njia za
kuyatatua.
Kwa upande wake mmoja wa wananchi waliotembelea banda
la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Nassor Juma alisema kuwa maadhimisho hayo
yamemsaidia kufahamu zaidi kuhusu fursa za elimu zinazopatikana nje ya mfumo wa
kawaida na namna elimu hiyo inavyoweza kumsaidia mtu kujiendeleza kielimu.
Ushiriki wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania katika
maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi
unaonesha nafasi ya elimu katika kuwawezesha wananchi kupata maarifa na ujuzi
unaolenga kukidhi mahitaji ya jamii, huku ukisisitiza umuhimu wa kujifunza kwa
maendeleo na ustawi wa jamii.
Comments
Post a Comment