IPSIS yawarahisishia madiwani Dodoma kufanya maamuzi

Na. Lulu Luvanda, DODOMA

Mfumo wa Kimataifa wa Uandishi na Uwasilishaji wa Taarifa za Fedha (IPSIS) umeelezwa kuwa umepunguza ugumu wa uandishi na uchakataji wa taarifa za fedha katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, huku ukirahisisha uwasilishaji wa hesabu na kuwawezesha madiwani kufanya maamuzi kwa uelewa zaidi.

 


Akizungumza wakati wa mkutano maalumu wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma ililofanyika katika ukumbi wa mikutano ya halmashauri Diwani wa Kata ya Miyuji, Ringo Iringo alisema kuwa  mfumo huo ni muhimu kwa Jiji la Dodoma kutokana na shughuli nyingi za kiuchumi na miradi mbalimbali ya maendeleo na ongezeko la shughuli za kifedha zinazohitaji usimamizi madhubuti.

Alisema kuwa mfumo wa IPSIS umeleta urahisi katika uandishi na uwasilishaji wa taarifa za kifedha, pamoja na kufanya mchakato wa kuchakata taarifa kuwa mwepesi na hivyo kusaidia viongozi kupata taarifa zinazoweza kuwa msingi wa kufanya maamuzi kwa wakati.

“Kwa sababu hiyo, IPSIS ni mfumo mzuri katika uandishi wa taarifa za kifedha kwa sababu unatoa urahisi katika uwasilishaji, uchakataji na kufanya maamuzi,” alisema Iringo.

Kwa upande wake, Prof. Davis Mwamfupe, Diwani wa Kata ya Madukani alisema kuwa mfumo huo wa kimataifa umechangia kurahisisha uelewa wa taarifa za hesabu zilizowasilishwa kwa baraza, jambo linalowawezesha madiwani kutekeleza wajibu wao wa kusimamia matumizi ya rasilimali za halmashauri.

 


Prof. Mwamfupe aliwataka wajumbe wa baraza kuwa na imani na Kamati ya Fedha na Utawala pamoja na wataalamu waliohusika katika kuandaa taarifa hiyo, akieleza kuwa utaalamu wao umesaidia kuhakikisha taarifa inawasilishwa kwa utaratibu unaoeleweka.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Tambukareli,  Clinton Manzi aliishukuru Kamati ya Fedha na Utawala pamoja na wataalamu waliohusika katika uandaaji wa taarifa za fedha, akisema kuwa ameshuhudia namna taarifa hiyo ilivyochakatwa kwa urahisi na kwa muda mfupi kutokana na matumizi ya mfumo wa IPSIS.

Hatua hiyo ilipelekea baraza la madiwani kuipokea taarifa ya ufungaji wa hesabu kwa kura za ndiyo, ikiwa ni ishara ya kuunga mkono taarifa iliyowasilishwa baada ya kupitia mchakato wa uchambuzi na majadiliano.

 

Comments

Popular Posts

Zahanati ya Chihoni Medical Center yazinduliwa Dodoma, wagonjwa 1,313 wahudumiwa

Kamati ya Fedha na Utawala Jiji la Dodoma yaridhishwa utekelezaji miradi ya maendeleo

Jiji la Dodoma lafaulisha kwa 91.23% Mtihani wa Darasa la Saba 2026