Wilaya ya Dodoma kutumia vyombo vya habari katika kampeni ya dhidi ya chanjo ya Polio
Na. Coletha Charles, NKUHUNGU
Wilaya
ya Dodoma imeweka mkakati wa kutumia vyombo vya habari, viongozi wa dini, shule
na kampuni za simu ili kuwahamasisha wazazi kuwapeleka watoto kupata chanjo
salama dhidi ya ugonjwa wa Polio, lengo likiwa ni kutokomeza kabisa hatari ya
maambukizi ya ugonjwa huo.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa zoezi hilo katika Shule ya Msingi Nkuhungu, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri, alisema kuwa vipindi vya redio na televisheni, hususani vipindi vya asubuhi, vitatumika kutoa elimu kwa wananchi na kujibu maswali kuhusu umuhimu na usalama wa chanjo hiyo.
Alisema
kuwa viongozi wa dini nao wamepewa nafasi muhimu katika uhamasishaji huo,
kutokana na ushawishi wao katika jamii na uwepo wa watoto katika maeneo ya
ibada, ikiwemo ‘Sunday Schools’, madrasa na jumuiya mbalimbali za kidini.
“Tumeona
pia kupitia eneo hilo kila mtoto wa Tanzania apate nafasi ya kupata chanjo
hiyo. Tumewahamasisha shule zote, kamati na bodi za shule kufikisha ujumbe kwa
wazazi. Pia tumeandaa ujumbe mfupi kwa kushirikiana na Vodacom, Tigo na Airtel
ili kuwafikishia wananchi taarifa kuhusu zoezi hili kupitia simu zao,” alisema
Alhaj Shekimweri.
Aidha, shule zimeingizwa katika mpango huo wa uhamasishaji, ambapo alisema wasimamizi wapatao 911 walioshiriki katika semina ya mitihani wamepewa maelekezo ya kuhakikisha kamati na bodi za shule zinawafikishia wazazi taarifa kuhusu zoezi hilo.
Kwa
upande wake, Afisa kutoka Wizara ya Afya, Idara ya Kinga sehemu ya Elimu ya
Afya, Magdalena Dinawi, alisema kuwa lengo la kampeni hiyo ni kuongeza na
kuimarisha kinga ya watoto dhidi ya virusi vya Polio aina ya pili, kuzuia
maambukizi kwa binadamu kupitia mazingira na kuhakikisha Tanzania inaendelea
kuwa nchi isiyo na maambukizi ya Polio.
“Natoa
wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha mtoto anapata chanjo hata kama tayari
ameshapata chanjo ya Polio kliniki au katika kampeni zilizopita. Chanjo ni
kinga, mpe chanjo, mlinde mtoto. Pia chanjo hii inatolewa bila malipo katika
vituo vya kutolea huduma za afya, nyumba kwa nyumba, tutatoa pia katika nyumba
zetu za ibada, vituo vya mabasi, sokoni na maeneo yote ya mikusanyiko ambapo
anapatikana mtoto chini ya miaka 10,” alisema Dinawi.
Nae, Mkazi wa Kata ya Nkuhungu, Mtaa wa Itega, Ally Hassan aliwasihi wazazi wenzake kutopuuza huduma hiyo inayotolewa bure na badala yake wawapeleke watoto wao ili kulinda afya na maisha yao ya baadaye.
“Natoa
wito kwa wazazi na walezi wahakikishe mtoto anapata chanjo hata kama tayari
alishapata chanjo ya Polio kliniki au katika kampeni zilizopita. Kupata chanjo
katika kampeni hii kunaongeza na kuimarisha kinga ya mwili na hivyo kumpa mtoto
ulinzi dhidi ya virusi vya polio vinavyoweza kuwepo kwenye mazingira” alisema.
Comments
Post a Comment