Wilaya ya Dodoma kuchanja watoto zaidi ya laki 2 chanjo ya Polio

Na. Coletha Charles, NKUHUNGU

 

Wilaya ya Dodoma imejipanga kuchanja watoto 207,096 chini ya miaka 10 dhidi ya ugonjwa wa Polio, sawa na asilimia 21 ya lengo la mkoa mzima, ikiwa ni utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya kujikinga na mlipuko wa ugonjwa huo.



Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, iliyofanyika katika Shule ya Msingi Nkuhungu, Kata ya Nkuhungu Halmshauri ya Jiji la Dodoma Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri alisema kuwa wilaya hiyo imekamilisha maandalizi yote ya kimkakati kupitia vikao vya ngazi tatu wataalamu, makundi ya hamasa na Kamati ya Afya ya Msingi ya Wilaya.

“Waliopewa kazi ya kuhamasisha, wafanye kazi hiyo ya uhamasishaji kikamilifu. Na kwa bahati njema, kama ambavyo tumeona hapa, wanatoka kwenye ngazi ya jamii, kwa hiyo wanafahamu namna ya kushirikiana na jamii. Tumepewa lengo la kuchanja watoto 207,096,” alisema Alhaj Shekimweri.

Alitumia nafasi hiyo kubainisha kuwa nchi haina mgonjwa wa Polio kwa sasa, hatua hiyo ni maelekezo ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuendelea kulinda afya za watoto. Aidha, alisisitiza kuwa zoezi hilo linapaswa kufanyika kwa ufanisi ili kuhakikisha hakuna dosari.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Nkuhungu, Mwl. Rogathe Makupa alisema kuwa zoezi la chanjo shuleni hapo limekwenda vizuri, ambapo kati ya wanafunzi 2,957, wanafunzi 1,360 ni walengwa wamepatiwa chanjo ya Polio.



“Niwaase wazazi ambao bado watoto wao hawajaweza kupatiwa chanjo, waweze kuwaleta watoto ili waweze kupatiwa chanjo hii ya Polio. Lakini pia kuna wauguzi wanapita mtaani kwa ajili ya zoezi hili zima la chanjo. Kwa hiyo tunaomba

tushirikiane nao katika zoezi zima la kufanikisha utoaji wa chanjo ya Polio,” alisema Mwl. Makupa.

Naye, Diwani wa Kata ya Nkuhungu, Julius Machea alisema kuwa anampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa chanjo hizo ili kuwalinda watoto wa taifa la kesho.

Kwangu mimi, niendelee tu kusititiza wananchi wote, wahudumu, walezi, wazazi, tuendelee kuleta watoto ili waweze kupata chanjo. Watu wote waone umuhimu wa jambo hili kwa uzito," alisema Machea.

Hata hivyo, Mkazi wa Nkuhungu Halmshauri ya Jiji la Dodoma, Rosemary Joseph aliwasihi wazazi ambao bado hawajawapeleka watoto wao kupata chanjo kufanya hivyo, akisisitiza kuwa chanjo ni muhimu katika kuwalinda watoto dhidi ya magonjwa.

Nawashauri wazazi wenzangu wawapeleke watoto kupata chanjo ili ziweze kuwalinda watoto wetu. Pia ninamshukuru Mungu kwa kutuwezesha kupata chanjo. Pia naishukuru serikali na Mama Samia kwa kuhakikisha chanjo zinawafikia watoto wetu. Kwa kweli nimefurahi kwa sababu nilipomleta mtoto wangu mwingine shuleni, nilielezwa kuwa mtoto huyu pia anaweza kupata chanjo hapa,” alisema Joseph.

Kwa ujumla, serikali imewataka wazazi na walezi katika Wilaya ya Dodoma kutumia fursa hiyo kuhakikisha watoto walio chini ya miaka 10 wanapata chanjo ya Polio, huku ikisisitiza kuwa ushirikiano wa jamii, viongozi na wahudumu wa afya ni muhimu katika kufanikisha kampeni hiyo na kuzuia kurejea kwa ugonjwa huo nchini.

MWISHO

 

Comments

Popular Posts

Vijana watakiwa kujiendeleza nje ya mfumo rasmi

NGOs zatakiwa kuzingatia uwazi na uwajibikaji Dodoma

Uendelevu wa NGOs wapatiwa msukumo wilayani Dodoma