TAKUKURU YAIBUKA NA PROGRAM YA USHIRIKI WANANCHI KUKABILI VITENDO VYA RUSHWA
Na Tabitha Joshua, CHANG’OMBE
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa
wa Dodoma imeanzisha programu iitwayo TAKUKURU Rafiki inayolenga kuongeza
ushiriki wa wananchi katika kukabili vitendo vya rushwa kwa jamii.
Afisa Uchunguzi wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma, Michael Sanga |
Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Uchunguzi wa TAKUKURU
Mkoa wa Dodoma, Michael Sanga katika kikao kilichofanyika katika Ofisi ya Afisa
Mtendaji Kata ya Chang’ombe iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Sanga alisema “TAKUKURU Rafiki ipo kwa lengo la
kufikia wananchi kwa karibu na kutatua kero zao wenyewe ambazo zinapatikana
katika idara zote, zinazopatikana katika kata hii. Vikao vyote vinavyohusu
TAKUKURU Rafiki vinafanywa katika ngazi ya kata Mwenyekiti wake ni diwani wa
kata na katibu wake anakuwa ni Afisa Mtendaji wa Kata”.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kata ya Chang’ombe,
Tunu Dachi aliishukuru Ofisi ya TAKUKURU kwa kuanzisha proramu hii kwasababu
imeweza kuondoa kero za wananchi katika kata hii. “Katika kikao hiki, tumeweza
kupata kero mbalimbali takribani kero tisa katika idara tofauti. Kero hizo
zilihusu maji, kero za vijana wa bodaboda, ubovu wa miundombinu katika soko
kipindi cha mvua na barabara, na pia tumehakikisha kuwa ndani ya mwezi mmoja
kero walizozitoa zitakuwa zimepewa majibu” alisema Dachi.
Alisema kuwa katika kikao hicho, kamati ndogo
imechaguliwa ambayo ina mwenyekiti, katibu na mtendaji kwa lengo la kuharakisha
kushugulikia na kutatua kero za wananchi.
Mwenyekiti aliyeteuliwa katika kamati ndogo, Jafari
Musa Athumani alisema kuwa amefurahishwa na juhudi za TAKUKURU Rafiki kutoa
elimu ya mapambano dhidi ya rushwa na kutatua kero za wananchi. “Ni vizuri kwa
TAKUKURU jinsi walivyotoa elimu kwasababu watu wengi hawaelewi juu ya jambo
hilo na pia ni vizuri kuwa watu wametoa kero zao ili ziweze kushughulikiwa”
alisema Mwenyekiti Athumani.
Mwenyekiti huyo aliwataka wananchi kutokuwaogopa
TAKUKURU badala yake badala yake kuwapa ushirikiano mkubwa kwa kutoa taarifa za
vitendo cha rushwa katika Kata. “Kwa hatua hii taifa litafika mbali kwasababu
itakuwa imeweza kutatua yale matatizo ambayo yameweza kuharibu uhusiano kwenye
jamii nzima” alisema Athumani.
Kikao hicho kilihudhuriwa na wafanyabiashara,
wananchi, viongozi wa dini, wanasiasa, viongozi wa serikali za mitaa, Chama Cha
Mapinduzi na wadau mbalimbali.
MWISHO
Comments
Post a Comment