Shilingi 8,318,810,005 zatolewa kuboresha sekta ya Elimu Dodoma
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WILAYA ya Dodoma imepokea shilingi 8,318,810,005 kwa
ajili ya kuboresha sekta ya elimu zikihusisha elimu bila malipo na ujenzi wa
miundombinu ya elimu kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kufundishia na
kujifunzia.
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Wilaya ya Dodoma,
Sakina Mbugi alipokuwa akisoma Risala ya Utii kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa Mbio za Mwenge wa
Uhuru Wilaya ya Dodoma katika uwanja wa Shule ya Msingi Kizota jijini Dodoma.
Alisema kuwa katika kipindi cha Julai, 2025 hadi Aprili,
2026 Wilaya ya Dodoma ilipokea shilingi 8,318,810,005 kwa ajili ya kuboresha
sekta ya elimu. Alisema kuwa kati ya fedha hizo, shilingi 3,777,397,654 ni kwa
ajili ya elimu bila malipo kwa shule za Awali, Msingi na Sekondari na shilingi 4,541,412,351 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu. ”Mheshimiwa Rais, kwa Kuboresha mazingira ya kujifunzia na
kufundishia, ufaulu umepanda katika shule za msingi kutoka asilimia 93.2 mwaka
2024 hadi asilimia 94.3 mwaka 2025. Pia, jumla ya
wanafunzi 13,971 wameandikishwa mwaka 2026 kujiunga na darasa la awali sawa na
asilimia 71.9 na wanafunzi 21,724 darasa la kwanza sawa na asilimia 118.4.
Aidha, katika shule za sekondari udahili wa wanafunzi wa Kidato
cha Kwanza umeongezeka kutoka asilimia 89.6
mwaka 2025 hadi kufikia asilimia 93 mwaka 2026 na ufaulu umeongezeka kutoka
asilimia 85.6 mwaka 2024 hadi
asilimia 92.6 mwaka 2025”
alisema Mbugi.
Alisema kuwa mwaka 2028 kutakuwa na wanafunzi wa kidato cha Kwanza waliomaliza darasa
la Sita na darasa la Saba kwa pamoja. ”Hivyo, wilaya inatarajia kuwa na
wanafunzi wa Kidato cha Kwanza 37,155. Kutokana na ongezeko hili, kwa Mwaka
2026/2027 wilaya imetenga shilingi 3,956,990,000 kwa ajili ya ujenzi wa
miundombinu ya madarasa, matundu ya vyoo pamoja na utengenezaji wa viti na meza
kwa shule za sekondari” alisema Mbugi.
Mwenge wa Uhuru Mwaka 2026 unaongozwa na kaulimbiu
isemayo ‘Tanzania ni Yetu Sote,
Tushikamane kwa pamoja Kuleta
Maendeleo ’.
MWISHO
Comments
Post a Comment