Watoa huduma wapatiwa mafunzo ya Lishe kwa wajawazito

Na. Mwandishi wetu, DODOMA

Watoa huduma za afya wanaohudumia wajawazito katika kliniki za huduma za mama na mtoto (ANC) wamepatiwa mafunzo kuhusu utekelezaji wa utafiti unaolenga kuboresha huduma za lishe kwa wajawazito katika Jiji la Dodoma.



Mafunzo hayo yalijikita katika kuwaongezea uwezo watoa huduma kuhusu utoaji wa elimu na huduma za lishe kwa wajawazito, ikiwa ni pamoja na namna ya kukabiliana na changamoto ya upungufu wa damu wakati wa ujauzito.

Akifungua mafunzo hayo, Kaimu Mganga Mkuu wa Jiji la Dodoma, Victor Kweka aliwataka watoa huduma kutumia maarifa wanayoyapata katika mafunzo hayo katika kuboresha huduma zinazotolewa kwa wajawazito katika vituo vya afya.

“Utoaji wa elimu sahihi kuhusu lishe na matumizi ya virutubisho vya nyongeza ni sehemu muhimu ya kuhakikisha wajawazito wanapata huduma bora na salama katika kipindi chote cha ujauzito, hivyo mnatakiwa kuhakikisha kila mjamzito anapokuja kliniki anapewa elimu ya lishe na umuhimu wa kunywa dawa” alisema Kweka.

Kwa upande wake Afisa Lishe Jiji la Dodoma, Semeni Eva Juma alisema kuwa kuna umuhimu wa akina mama wajawazito kuwahi kliniki wakiwa na ujauzito chini ya wiki 12 ambapo ataweza kupata elimu sahihi ili aweza kujifungua salama.



Miongoni mwa mada zilizotolewa ni lishe bora kwa mjamzito na upungufu wa damu, huduma za kuzuia na kujikinga na maradhi, umuhimu wa huduma za kliniki ya wajawazito (ANC), pamoja na utoaji wa virutubisho vya nyongeza kwa wajawazito.

Mafunzo hayo pia yalilenga kuwawezesha watoa huduma kutekeleza utafiti huo kwa ufanisi, huku wakizingatia taratibu za utoaji wa huduma na ukusanyaji wa taarifa zitakazosaidia katika kuboresha huduma za lishe kwa wajawazito.

Comments

Popular Posts

Polisi Kata waungana zoezi la Usafi wa Mazingira Dodoma

Kata ya Matumbulu wanufaika na Mil. 14.7 Maadhimisho ya Samia Day