Wanufaika wa mikopo ya 10% walishukuru Jiji la Dodoma

Na. Coletha Charles, DODOMA

 

Wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 isiyo na riba inayotolewa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma wameishukuru serikali kwa fursa hiyo, wakieleza kuwa imewawezesha kuanzisha miradi, kukuza biashara na kuongeza kipato.

 


Shukrani hizo zilitolewa katika kikao cha tathmini ya usimamizi na utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jiji la Dodoma kikilenga kuboresha huduma hiyo.

 

Mwenyekiti wa Kikundi cha Tupambane Vijana kilichopo Kata ya Majengo, Paschal Peter alisema kuwa mikopo hiyo imekuwa msaada mkubwa kwa kikundi chao, ambacho kimefanikiwa kupata fedha katika awamu mbili.

 

“Awamu ya kwanza tulikopa shilingi milioni 5, awamu ya pili shilingi milioni 10 na kurejesha kwa wakati, huku kwa sasa tukiwa tumeomba shilingi milioni 60.087 kwa ajili ya kununua bajaji,” alisema Peter.

 

Kwa upande wake, Katibu wa Kikundi cha Wining Star kilichopo Kata ya Ipagala, Julia Malaba aliishukuru halmshauri kwa kuwapa mkopo wa shilingi milioni 20 uliowawezesha kuanzisha mradi wa ufugaji wa kuku.

 


Akizungumzia mpango huo, Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii Jiji la Dodoma, Charity Sichona alisema kuwa wameweka mikakati ya kushirikisha benki, madiwani na maafisa maendeleo ya jamii katika kuwezesha vikundi.

 

“Tumepanga kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili vikundi vielewe taratibu na vigezo vya mikopo, pamoja na kupata msaada unaohitajika wakati wa kuandaa na kuwasilisha maombi,” alisema Sichona.

 


Mikopo ya asilimia 10 inatolewa kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa lengo la kuwawezesha kiuchumi, kukuza miradi ya uzalishaji, kujiajiri na kuongeza kipato kupitia shughuli mbalimbali za maendeleo.

MWISHO

Comments

Popular Posts

KATA YA CHAMWINO YATEKELEZA AGIZO LA USAFI WA MAZINGIRA

Mfumo wa NeST warahisisha utiaji saini mkataba wa HOTSAC, Dodoma