Mwenyekiti UWT Taifa awataka wanawake kuchangamkia mikopo ya Jiji la Dodoma
Na. Faraja Mbise. DODOMA
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT)
Taifa, Mary Chatanda amewataka wanawake wafanyabiashara wa Halmashauri ya Jiji
la Dodoma kuachana na mikopo ya Kausha damu na mwendokasi
inayowanyanyasa na kuwadhalilisha wanawake kutokana na muda wa marejesho na
kiwango cha riba kuwa kikubwa na hivyo kushindwa kujikwamua kiuchumi na kuwaongezea
umasikini zaidi.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Taifa, Mary Chatanda |
Kauli hiyo aliitoa wakati akizungumza
katika Uzinduzi wa Umoja wa Wanawake Wafanyabiashara Masoko yote katika Jiji la
Dodoma (UWAWAMA), uliofanyika Cathedral Social Hall, tarehe 01 Novemba, 2024.
Chatanda aliwataka wanawake
wafanyabiashara kuachana na mikopo ya kausha damu na kujiunga na vikundi ili
kupata mikopo ambayo inatolewa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma. "Serikali
ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluh Hassan
imerejesha utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake, vijana na
watu wenye ulemavu kwa utaratibu ulioboreshwa zaidi ikiwemo kutumia benki kwa halmashauri
kumi za majaribio zikiwemo za Dodoma" alisema Chatanda.
Kuhusu mikopo ya kausha damu, aliwataka
wafanyabiashara kuachana nayo kwasababu inarudisha uchumi wa nchi nyuma na
mwanamke anashindwa kujikwamua kiuchumi kutokana na masharti magumu ya riba na
muda uliowekwa katika mikopo hiyo. "Sasa nawahimiza kuchangamkia fursa ya
mkopo usio na riba tuliyopewa na serikali na kuondokana na mikopo ya kausha damu,
ujinga na mwendokasi inayowanyanyasa na kuwadhalilisha wanawake kutokana na
utaratibu wa mikopo hiyo ukiwemo muda wa marejesho na kiwango kikubwa cha riba
kuwa kikubwa hivyo badala ya kujikwamua kiuchumi inaongeza umaskini zaidi"
alisisitiza Chatanda.
Katika kuhamasisha wanawake walengwa wa
mikopo, alitoa rai kwa viongozi wanawake kuhamasisha wachangamkie fursa ya
mikopo inayotolewa na serikali. "Natoa wito kwa viongozi wanawake
kuhamasisha walengwa wa mikopo hii wachangamkie fursa ya mikopo inayotolewa na
serikali yao" alisisitiza Chatanda.
Aidha, aliwashukuru wanawake wa nchi nzima
kuitikia wito wa kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura katika Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa uliofanyika tarehe 11 hadi 20 Oktoba, 2024.
"Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) inaonesha
wanawake walioandikishwa ni asilimia 51.29 na asilimia 48.71 ni wanaume. Asanteni
sana wanawake kwa kuiheshimisha serikali, kiongozi wetu mkuu wa nchi pamoja na
mimi mwenyekiti wenu ambaye wakati wa ziara zangu zote nimekuwa nikiwasihi
wanawake na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kwenda kujiandikisha"
alieleza Chatanda.
Uzinduzi wa umoja wa wanawake
wafanyabiashara masoko yote katika Jiji la Dodoma ulihudhuriwa na wanawake wa
masoko mbalimbali kama Soko kuu la Job Ndugai, Sabasaba, Majengo, Machinga na
Bonanza. Pia na vikundi mbalimbali kama Wanawake na Samia, wanawake na Nyerere,
Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Dodoma Jiji (JUWAKIDO).
MWISHO
Nouma sana mwandishi🔥🔥🔥🔥🔥
ReplyDelete