Hai DC kuimarisha miradi ya kimkakati baada ya kujifunza Dodoma

Na. Mwandishi wetu, DODOMA

 

Halmashauri ya Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro imejifunza mbinu za kubuni na kuendeleza miradi ya kimkakati baada ya kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo katika Jiji la Dodoma.

 


Ziara hiyo ilihusisha Soko la Job Ndugai, Soko la Wazi la Machinga, Chinangali Park, maegesho ya malori Nala, Jengo la Kitenga Uchumi Mtumba pamoja na Kituo Kikuu Cha Mabasi Dodoma.

 

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Edmund Rutaraka alisema kuwa ziara hiyo imewapa fursa ya kuona namna miradi mbalimbali inavyotekelezwa na kupata uzoefu wa kuboresha miradi katika halmashauri yao.

 

“Tumejifunza umuhimu wa kuwa na maeneo maalumu kwa shughuli mbalimbali, ikiwemo biashara, maegesho ya magari makubwa na huduma za usafiri, ili kuboresha huduma kwa wananchi kulingana na mahitaji yao,” alisema Rutaraka.

 


Kwa upande wake, Diwani wa viti maalumu wa Tarafa ya Masama, Lightness Laizer alisema kuwa wamejifunza mbinu mbalimbali za kuendeleza miradi, ikiwemo namna ya kuboresha maeneo ya biashara na kuwapa wafanyabiashara mazingira yanayofaa.

 

“Tumetembelea mradi wa Soko la Machinga na tumeona jinsi gani vijana walivyo na ubunifu. Sisi pia tuna eneo letu Hai, na tukirudi tutakwenda kufanya kile tulichokiona hapa kwenye Soko la Machinga,” alisema Laizer.

 

Nae, Afisa Biashara wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Christina Lyimo alisema kuwa ziara hiyo imewawezesha kuona miradi inayotoa huduma mbalimbali kwa wananchi na kujifunza namna ya kuendeleza uwekezaji wa miundombinu.

 

“Ukiangalia Chinangali Park kwa kweli panavutia. Tumeona viwanja vya michezo, maeneo ya wazi ambayo watu wanakodisha kwa ajili ya matamasha, swimming pool na sehemu za watoto kucheza. Tunaona wenzetu wamewekeza katika sekta mbalimbali,” alisema Lyimo.

 

Miradi hiyo imewawezesha wajumbe wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai kujifunza namna ya kuendeleza maeneo ya biashara, burudani na usafiri ili kuboresha huduma kwa wananchi na kuongeza fursa za uwekezaji katika halmashauri yao.

Comments

Popular Posts

Kata ya Matumbulu wanufaika na Mil. 114.7 Maadhimisho ya Samia Day

Samia Day 2026 yaibua vipaji vya michezo Kata ya Matumbulu