Wananchi Kata ya Msalato watakiwa kufanya usafi kama utamaduni

Na. Mwandishi wetu, MSALATO

Wafanyabiashara na wananchi katika eneo la Mnada wa Msalato wametakiwa kuufanya usafi kuwa sehemu ya maisha ya kila siku, badala ya kusubiri siku maalum za usafi.

 


Wito huo ulitolewa wakati wa zoezi la usafi wa mazingira lililofanyika katika eneo hilo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Samia Day, ambapo wananchi walishiriki kusafisha mazingira ya mnada.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Alicia Anthony, mchumi wa Kanda ya utoaji huduma Namba Sita ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, alisema kuwa usafi ni muhimu sawa na chakula, hivyo wananchi wanapaswa kuuzingatia katika majumbani, maeneo ya kazi na biashara.

“Mazingira safi humfanya mteja kujisikia salama na kuwa na imani na bidhaa au huduma anayopewa, niwapongeza wafanyabiashara kwa kushiriki zoezi hili na niwatake kulifanya kuwa utamaduni wa kila siku,” alisema Anthony.

Kwa upande wake Balozi wa Mtaa wa Chikole, Joyce Jackson alisema kuwa wananchi wameitikia vizuri wito wa kufanya usafi katika maadhimisho ya Samia Day, hali iliyosaidia kubadilisha mwonekano wa eneo la mnada. Alisema kuwa maeneo ambayo awali yalikuwa yamejaa taka mbalimbali sasa yamekuwa safi, huku akisisitiza kuwa bado kuna haja ya kuongeza juhudi ili usafi huo udumishwe.

Nae Katibu wa Nyamachoma katika Mnada wa Msalato, Haji Mauridi Chiwiche alisema kuwa zoezi hilo limetoa mabadiliko katika mazingira ya mnada, huku akishukuru viongozi kwa kuhamasisha wananchi kushiriki.

Aidha, aliishukuru serikali kwa ujenzi wa mabanda na maboresho yanayoendelea katika eneo hilo, akisema kuwa hatua hizo zinasaidia kufanya mnada kuwa katika mazingira bora zaidi kwa wafanyabiashara na wateja.

Zoezi hilo la usafi limefanyika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Samia Day, likilenga kuhamasisha wananchi kuendelea kutunza mazingira na kufanya usafi kuwa utamaduni wa kila siku.





Comments

Popular Posts

Polisi Kata waungana zoezi la Usafi wa Mazingira Dodoma

DC Shekimweri afanya ukaguzi wa usafi Kata ya Kizota

Dodoma kuanza awamu ya pili ya Kampeni ya Chanjo ya Polio tarehe 29 Septemba, 2026