Kizota yaadhimisha Samia Day, ikitoa elimu ya Lishe kwa Umma
Na. Mwandishi wetu, KIZOTA
Kata ya Kizota, Halmashauri ya Jiji la Dodoma
imeadhimisha Samia Day kwa kutoa elimu ya afya na lishe kupitia Siku ya Afya na
Lishe ya Mtaa (SALIKI), kufanya usafi katika Stendi ya Mnada Mpya, pamoja na
kuwaelimisha wananchi kuhusu miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali
katika kata hiyo.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Polisi Kata ya Kizota, Inspekta Baraka Simbabawe alitoa elimu kuhusu umuhimu wa lishe bora, akitaja makundi muhimu ya vyakula kuwa ni nafaka na mizizi, jamii ya kunde, vyakula vinavyotokana na wanyama, mboga za majani na matunda. Alisema kuwa ulaji wa vyakula kutoka katika makundi hayo husaidia kujenga mwili na kuimarisha afya, huku lishe duni ikichangia changamoto kama utapiamlo, upungufu wa damu na mwili kukosa nguvu.
Inspekta Simbabawe aliwasisitiza wazazi kuhakikisha
watoto wanapata chakula bora chenye virutubisho muhimu ili waweze kukua na
kuimarika kiafya. Pia aliwahimiza wanawake wajawazito kuzingatia lishe bora na
mlo kamili unaojumuisha makundi mbalimbali ya vyakula kwa ajili ya afya ya mama
na ukuaji mzuri wa mtoto aliye tumboni.
Akielezea utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika
Kata ya Kizota, Afisa Mtendaji wa Kata ya hiyo, Aidan Libenanga alisema kuwa serikali
imeendelea kuboresha miundombinu na huduma za kijamii, ikiwemo ujenzi wa
barabara za lami na changarawe na ujenzi wa Stendi ya Mnada Mpya. Alitaja pia
ujenzi wa Shule ya Msingi Mahungu wenye thamani ya Shilingi milioni 321, Kituo
cha Afya Kizota chenye thamani ya shilingi milioni 455 pamoja na maabara mbili
katika Shule ya Sekondari Kizota zenye thamani ya shilingi milioni 37.
Alisema kuwa katika mwaka wa fedha 2026/2027, Kata ya
Kizota imeingiziwa kiasi cha Shilingi milioni 87.3 kwa ajili ya kutekeleza
shughuli mbalimbali za maendeleo, ikiwemo kutengeneza madawati 164
yatakayogawiwa katika shule zilizopo ndani ya kata, pamoja na uchimbaji wa
kisima cha kisasa kwa ajili ya wananchi wa kata hiyo na ujenzi wa vyumba viwili
vya madarasa katika Shule ya Msingi Mahungu.
Maadhimisho hayo yalihitimishwa kwa zoezi la usafi wa
mazingira katika Stendi ya Mnada Mpya, lililoshirikisha viongozi na wananchi.
Zoezi hilo lililenga kuhamasisha jamii kuendelea kutunza mazingira na kushiriki
kikamilifu katika shughuli za maendeleo, huku wananchi wakikumbushwa umuhimu wa
kutunza na kutumia vizuri miundombinu inayotekelezwa kwa ajili ya kuboresha
huduma na maisha yao.
Comments
Post a Comment