JIJI LA DODOMA LAITANDIKA CHAMWINO DC 38-9 MPIRA WA PETE SHIMISEMITA
Na. Mwandishi wetu, MBEYA
Timu ya Wanawake ya Mpira wa Pete ya Halmashauri ya
Jiji la Dodoma imeitandika Timu ya Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino magoli 38-9
ikiwa ni muendelezo wa juhudi zake za kufukuzia ubingwa katika mashindano ya
SHIMISEMITA yanayoendelea jijini Mbeya.
Akizungumzia mchezo huo, Afisa Michezo wa Jiji la
Dodoma, Neema Kilongola mara baada ya mchezo huo kutamatika katika viwanja vya
Shule ya Sekondari Mbeya alisema kuwa timu yake imejipanga kushindana. Alisema
kuwa timu hiyo inaendelea vizuri katika mashindano hayo na anaamini kuwa
ubingwa wa SHIMISEMITA bado utaendelea kubaki mikononi mwao. “Tunaendelea
vizuri na mashindano. Tunaamini ubingwa bado utabaki kwetu kwa sababu sisi ndio
mabingwa wa mashindano haya. Hivyo, tunataka kuhakikisha tunautetea ubingwa
wetu” alisema Kilongola.
Aliongezea kuwa ushindi wa magoli 38–9 umeipa Halmashauri
ya Jiji la Dodoma mwanzo mzuri wa kampeni yake ya kutetea ubingwa, huku
matarajio yakiongezeka kwa mashabiki kuona kama timu hiyo itaendelea na kiwango
hicho katika michezo inayofuata.
Comments
Post a Comment