Siku ya Afya na Lishe Mtaa wa Bochela yawa fursa ya chanjo na elimu kwa jamii
Na. Mwandishi wetu , NKUHUNGU
Wananchi
wa Mtaa wa Bochela, Kata ya Nkuhungu, jijini Dodoma, wameungana kuadhimisha
Siku ya Afya na Lishe, ambapo wamepatiwa elimu ya lishe pamoja na huduma za
chanjo kwa watoto wadogo.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Muuguzi kutoka Jiji la Dodoma anayehudumu katika Kituo cha Afya Nkuhungu, Getrude Modest, alisema kuwa zoezi hilo ni sehemu ya kuwafikishia wananchi huduma za afya, hususan chanjo kwa watoto wenye umri wa miezi tisa na mwaka mmoja.
Alisema
kuwa chanjo hizo zinatolewa bila malipo, huku akiwapongeza wazazi na walezi kwa
kuitikia kwa wingi na kuhakikisha watoto wao wanapata huduma hizo kwa wakati.
Kwa
upande wake, mwananchi wa Mtaa wa Bochela, Rehema Hafidhi, alisema kuwa zoezi hilo ni muhimu kwa jamii kwa
kuwa linawawezesha wazazi kupata elimu ya afya na lishe pamoja na kupata huduma
muhimu karibu na maeneo yao ya makazi.
Aliomba viongozi na wataalamu wa afya kuendelea kuandaa matukio kama hayo mara kwa mara ili wananchi wengi zaidi waweze kufikiwa, akisisitiza pia umuhimu wa kuwafikia wajawazito na kuwapatia elimu na huduma zinazohusiana na afya ya mama na mtoto.
Comments
Post a Comment