Wananchi wapewa elimu ya Afya na Lishe bora Nkuhungu

Na. Mwandishi wetu, DODOMA

 

Wananchi wa Mtaa wa Bochela, Kata ya Nkuhungu, jijini Dodoma, walipatiwa elimu kuhusu afya na lishe bora, hususan namna ya kuandaa chakula chenye virutubisho muhimu kwa watoto kuanzia umri wa miezi sita hadi miaka mitano.

 


Elimu hiyo ilitolewa wakati wa Siku ya Afya na Lishe ya Mtaa (SALiKI) ambapo kina mama walielekezwa umuhimu wa kumpatia mtoto chakula chenye mchanganyiko wa makundi mbalimbali ya vyakula kwa ajili ya ukuaji na afya bora.

 

Akitoa elimu hiyo, Mtaalamu wa Lishe kutoka Kituo cha Afya Nkuhungu, Getruda Modesti aliwaelekeza wazazi kuhakikisha watoto kuanzia miezi sita wanapatiwa vyakula vyenye virutubisho kutoka katika makundi muhimu ya vyakula, huku wakiendelea kunyonya hadi kufikia umri wa miaka miwili.

 

Makundi hayo yalihusisha mboga za majani, matunda yenye vitamini na madini, jamii ya mikunde, vyakula vya wanga vinavyoupa mwili nguvu, pamoja na vyakula vya kujenga mwili vyenye protini kutoka katika vyanzo mbalimbali, ikiwemo vyakula vitokanavyo na wanyama.

 

Aidha, kina mama walifundishwa namna ya kuandaa uji wenye virutubisho vya kutosha ili kuwasaidia watoto kupata lishe bora, hamu ya kula na kukua wakiwa na afya njema.

 

Katika hatua nyingine, wajawazito walipatiwa elimu kuhusu umuhimu wa kutumia dawa za folic acid kwa ushauri wa wataalamu wa afya, kwa lengo la kusaidia ukuaji mzuri wa mtoto akiwa tumboni.

 

Elimu hiyo ililenga kuongeza uelewa wa wazazi na walezi kuhusu umuhimu wa lishe bora na kuhakikisha watoto wanapata mlo wenye virutubisho muhimu katika hatua mbalimbali za ukuaji wao.

Comments

Popular Posts

Jiji la Dodoma Biashara saa 24, usafi saa 24

Mvua za El Nino: DC Shekimweri awaasa wananchi wa Dodoma Kuchukua Tahadhari

Wananchi Dodoma wahimizwa kufanya usafi wa Mazingira kila siku