Mvua za El Nino: DC Shekimweri awaasa wananchi wa Dodoma Kuchukua Tahadhari
Na. Mwandishi wetu, NZUGUNI
Wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi wametakiwa
kuchukua tahadhari mapema dhidi ya mvua za El Nino, ikiwemo kuepuka maeneo
yanayoweza kukumbwa na mafuriko na kuhakikisha usalama wa familia zao.
Akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi wa bwawa la kuvunia maji ya mvua katika viwanja vya Dkt. John Malecela (Nanenane), Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri alisema kuwa wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi wanapaswa kuzingatia tahadhari zinazotolewa na mamlaka.
Alisema kuwa wananchi wanaoishi mabondeni, karibu na
mito na maeneo yanayoweza kuathiriwa na mafuriko wanapaswa kuwa makini na
kuchukua hatua mapema ili kuepusha madhara yanayoweza kusababishwa na mvua
kubwa.
Aidha, aliwataka wananchi kuhakikisha mifereji na njia
za maji hazizibwi kwa taka, akieleza kuwa hali hiyo inaweza kuzuia mtiririko wa
maji na kuongeza uwezekano wa kutokea kwa mafuriko katika maeneo ya makazi.
Katika ziara hiyo, alikagua hali ya bwawa hilo pamoja na miundombinu ya kuvunia na kuhifadhi maji ya mvua, huku akisisitiza umuhimu wa maandalizi ya mapema katika kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua.
Alisema kuwa usalama wa wananchi ni jukumu la pamoja,
hivyo aliwataka viongozi na wananchi kushirikiana, kufuatilia taarifa za hali
ya hewa na kuchukua hatua stahiki pindi wanapopata tahadhari kuhusu uwezekano
wa mvua kubwa.
Comments
Post a Comment