Mtaa wa Bochela wapewa elimu kupinga ukatili wa kijinsia

Na. Mwandishi wetu, NKUHUNGU


Wananchi wa Mtaa wa Bochela, Kata ya Nkuhungu, jijini Dodoma, walipatiwa elimu kuhusu ukatili wa kijinsia, aina zake, madhara pamoja na umuhimu wa kutoa taarifa kuhusu vitendo hivyo katik maadhimisho ya Siku ya Afya na Lishe ya Mtaa (SALiKI).


Akizungumza wakati wa kutoa elimu hiyo, Inspekta Amina Shabani kutoka Polisi Kata ya Nkuhungu, alieleza kuwa ukatili wa kijinsia unahusisha matendo mbalimbali yanayosababisha mtu mateso au madhara kwa njia ya kimwili, kingono, kiuchumi au kihisia.


Alifafanua kuwa miongoni mwa aina za ukatili wa kijinsia zilizotolewa elimu zilikuwa ukatili wa kimwili, ukatili wa kingono ikiwemo kulawitiwa, ukatili wa kiuchumi pamoja na ukatili wa kihisia.

Aliwahimiza wananchi kuwa na uelewa kuhusu vitendo vya ukatili wa kijinsia na kutokaa kimya wanapobaini matukio hayo, badala yake wanatakiwa kutoa taarifa kwa vyombo husika ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.


Aidha, alisisitiza umuhimu wa jamii kushirikiana katika kuzuia vitendo vya ukatili na kulinda watoto, wanawake pamoja na makundi mengine yaliyokuwa katika mazingira hatarishi.

Elimu hiyo ilitolewa ikiwa ni sehemu ya shughuli za uhamasishaji kwa wananchi wa Mtaa wa Bochela kwa lengo la kuongeza uelewa wa jamii kuhusu namna ya kutambua, kuzuia na kutoa taarifa za vitendo vya ukatili wa kijinsia.






Comments

Popular Posts

Mvua za El Nino: DC Shekimweri awaasa wananchi wa Dodoma Kuchukua Tahadhari

Jiji la Dodoma Biashara saa 24, usafi saa 24

Wananchi Dodoma wahimizwa kufanya usafi wa Mazingira kila siku