CCTV Camera zaimarisha usalama Jiji la Dodoma
Na. Mwandishi wetu, DODOMA
Ufungaji wa kamera za CCTV katika maeneo mbalimbali
umeendelea kuimarisha usalama, utii wa sheria za barabarani na ulinzi katika Jiji
la Dodoma, huku madiwani wakipokea taarifa ya utendaji kazi wa TEHAMA.
Kauli hiyo ilitolewa na Kaimu Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Vincent Oderо wakati akiwasilisha taarifa ya
utendaji kazi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 katika mkutano wa Mwaka wa Baraza la
Madiwani uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa jiji hilo.
Alisema kuwa Mwaka wa Fedha 2024/2025, maeneo 35
yalipangwa kufungwa kamera za CCTV, ambapo manne yalifungwa na maeneo 31
yakabaki kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026, maeneo 31 yalipangwa kufungwa CCTV,
ambapo 26 yamekamilika na maeneo matano bado hayajafungwa.
“Katika utekelezaji wa mifumo ya TEHAMA, kwa mwaka wa
fedha 2024/2025, taasisi 287 kati ya 333 zilizopangwa zilifungiwa mifumo. Kwa
mwaka wa fedha 2025/2026, taasisi 179 kati ya 227 zilizopangwa zimefungiwa
mifumo. Hatua hizi zinaendelea kuongeza matumizi ya teknolojia,” alisema
Onderо.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Zuzu, Jenesta
Malingo, alisema kuwa uwepo wa CCTV kamera barabarani unasaidia wananchi
kufuata sheria bila kulazimishwa, huku ukirahisisha ufuatiliaji na udhibiti wa
matukio yanayoweza kuhatarisha amani na usalama.
Alisema kuwa Dodoma ina umuhimu wa kipekee kutokana na
kuwa Makao Makuu ya nchi, ambako kuna Bunge, viongozi mbalimbali wa kitaifa na
Ikulu, hivyo matumizi ya TEHAMA ni muhimu katika kuimarisha ulinzi na usalama.
“Naipongeza serikali, uongozi wa jiji na watendaji wa
Kitengo cha TEHAMA kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya katika kuhakikisha
matumizi ya teknolojia yanaimarika. Uwepo wa mifumo ya TEHAMA na kamera za CCTV
umeongeza ufanisi katika ulinzi na usalama na kuifanya Dodoma kuwa jiji la
kisasa,” alisema Malingo.
Madiwani walipokea taarifa hiyo ya utendaji kazi wa halmashauri,
ikiwemo utekelezaji wa shughuli za Kitengo cha TEHAMA katika Miaka ya Fedha
2024/2025 na 2025/2026, huku wakielezwa hatua zilizochukuliwa katika kuimarisha
mifumo ya kidijitali, usalama na matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma
kwa wananchi.
MWISHO
Comments
Post a Comment