GCU Jiji la Dodoma yapongezwa umahiri katika kuhabarisha Umma

Na. Mwandishi wetu, DODOMA

 

BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma limekipongeza Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kwa kazi nzuri ya kuhakikisha wananchi wanapata taarifa na habari kuhusu shughuli na utekelezaji wa majukumu ya halmashauri kwa wakati.


Pongezi hizo zilitolewa na Diwani wa Kata ya Mnadani, Mugendi Kerenge wakati akichangia kwenye mkutano wa Baraza la Madiwani kwa ajili ya kupokea na kuajdili taarifa ya utekelezaji wa kazi za halmashauri kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026, uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

 

Kerenge aliwapongeza wataalam wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kwa namna walivyokuwa wakitekeleza majukumu yao ya kuhabarisha umma kuhusu shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na halmashauri.

 

“Nawapongeza wataalam wetu wa habari kwa namna wanavyofanya kazi nzuri ya kuhabarisha umma kwa wakati. Wananchi wamekuwa wakipata habari mbalimbali kutoka katika maeneo yao. Mfano, mimi habari za kata yangu zimekuwa zikitolewa mara nyingi na kwa wakati hivyo kuwawezesha wananchi kufahamu kinachoendelea na mikakati tuliyonayo” alisema Kerenge.

 

Kwa upande wake, Afisa Habari katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Leah Mabalwe alisema kuwa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kina jukumu la kuhakikisha wananchi wanapata taarifa, habari na matangazo mbalimbali ya halmashauri kwa wakati ili wawe na uelewa wa kila jambo linalotekelezwa na serikali yao.

 

Mabalwe alisema kuwa kitengo hicho kitaendelea kushirikiana na viongozi na wataalam wa halmashauri katika kuhakikisha wananchi wanafahamishwa kwa usahihi na kwa wakati kuhusu shughuli za maendeleo, huduma na fursa zinazotolewa na halmashauri.

 

Alisema kuwa kuimarishwa kwa mawasiliano kati ya halmashauri na wananchi kutaendelea kuwa sehemu muhimu ya kuhakikisha umma unapata taarifa sahihi, kwa wakati na kupitia njia rasmi za mawasiliano za halmashauri.

Comments

Popular Posts

Kata ya Miyuji Yaongeza Kasi ya Usimamizi Wa Usafi wa Mazingira

Kata za Nkuhungu na Kizota zajiandaa kukabiliana na mvua za El Nino

Mwenyekiti Mtaa wa Karume, Kata ya Mnadani ahamasisha usafi