Ufaulu elimu ya msingi wapanda Jiji la Dodoma hadi 94.3%

Na. Mwandishi wetu, DODOMA

 

Ufaulu wa wanafunzi wa shule za msingi Jiji la Dodoma umeongezeka katika mitihani ya PSLE na SFNA, ukifikia asilimia 93.32 na 94.3 kwa Mwaka 2025, kutoka asilimia 89.15 na 88.9 Mwaka 2021.

 


Akizungumza wakati wa kuwasilisha taarifa ya utendaji kazi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026, kwenye mkutano wa Mwaka cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa jiji hilo. 

 

Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Vincent Odero alisema kuwa ongezeko hilo ni miongoni mwa mafanikio makubwa katika sekta ya elimu ya msingi, likionesha jitihada za halmashauri kuboresha elimu na kuongeza ufaulu wa wanafunzi.

 

“Ufaulu wa wanafunzi kwa miaka mitano kwa Darasa la Saba (PSLE) umeongezeka kutoka asilimia 89.15 kwa Mwaka 2021 hadi asilimia 93.32 Mwaka 2025. Aidha, ufaulu wa Darasa la Nne (SFNA) kwa miaka mitano umeongezeka kutoka asilimia 88.90 hadi asilimia 94.30, sawa na ongezeko la asilimia 5.4,” alisema Odero.

 

Akichangia taarifa hiyo, Diwani wa Kata ya Mnadani, Mugendi Kerenge alisema kuwa rasilimali zilizopo zitumike kuwapeleka walimu katika shule za pembezoni ili kuongeza zaidi kiwango cha ufaulu.

 


“Tumeongeza ufaulu hasa katika shule za msingi kwa asilimia tano, jambo ambalo ni hatua kubwa na ya kutia moyo katika kuboresha elimu. Tutoe rasilimali tulizonazo na kuzipeleka kwenye shule za pembezoni ili kupunguza tofauti ya upatikanaji wa walimu kati ya shule za mjini na zile za pembezoni,” alisema Kerenge.

 

Mafanikio hayo yanaweka msingi wa Jiji la Dodoma kuendelea kuboresha elimu ya msingi na kuongeza zaidi ufaulu wa wanafunzi katika miaka ijayo.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Kata ya Miyuji Yaongeza Kasi ya Usimamizi Wa Usafi wa Mazingira

Kata za Nkuhungu na Kizota zajiandaa kukabiliana na mvua za El Nino

Mwenyekiti Mtaa wa Karume, Kata ya Mnadani ahamasisha usafi