Ufaulu Elimu Sekondari wapanda Jiji la Dodoma

Na. Mwandishi wetu, DODOMA

 

Ufaulu wa mitihani ya taifa kwa wanafunzi wa sekondari Jiji la Dodoma umeimarika kwa Mwaka 2025/2026, ambapo Division I, II na III zikiongezeka.

 


Hayo yameelezwa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Vincent Odero wakati akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 katika Mkutano wa Mwaka wa Baraza la Madiwani uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa jiji hilo.

 

Alisema kuwa mwelekeo huo unaashiria maendeleo chanya katika sekta ya elimu ya sekondari, yakichangiwa na usimamizi mzuri wa elimu pamoja na juhudi kubwa za walimu katika kuboresha ufundishaji na kuongeza ufaulu wa wanafunzi.

 

“Wanafunzi waliofanya mtihani waliongezeka kutoka 6,526 Mwaka 2024/2025 hadi 7,104 Mwaka 2025/2026, huku ufaulu wa ‘Division’ I, II na III ukiongezeka na ‘Division’ 0 na IV ukipungua. Hii inaashiria mwelekeo chanya unaoendelea,” alisema Odero.

 

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Viwandani, Swalihina Athuman alisema kuwa walimu wamekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza ufaulu kwa kuwapatia wanafunzi muda wa ziada wa masomo na kuendesha kambi za masomo.

 

Alisema kuwa ushirikiano wa wazazi, walimu na Baraza la Madiwani umeendelea kuwa muhimu katika kusimamia maendeleo ya wanafunzi, huku wazazi wakihimizwa kuongeza ufuatiliaji wa watoto wanapokuwa nyumbani ili kuimarisha zaidi ufaulu.

 

“Tunatoa pongezi kwa walimu. Walimu wamefanya juhudi kubwa, wameongeza mazingira mazuri ya ufaulu kwa watoto kwa kutoa muda wao wa kuwasomesha na kuwafanya watoto wale wawe wanarejea mara kwa mara,” alisema Athuman.

 

Jiji la Dodoma lina jumla ya shule 72 za sekondari, zikiwemo shule 46 za serikali na shule 26 za binafsi, zenye wanafunzi 45,692. Kati yao, wanafunzi 38,839 wanasoma katika shule za serikali, wakiwemo wavulana 17,167 na wasichana 21,672, huku shule za binafsi zikiwa na wanafunzi 6,853, wakiwemo wavulana 3,656 na wasichana 3,197.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Kata ya Miyuji Yaongeza Kasi ya Usimamizi Wa Usafi wa Mazingira

Kata za Nkuhungu na Kizota zajiandaa kukabiliana na mvua za El Nino

Mwenyekiti Mtaa wa Karume, Kata ya Mnadani ahamasisha usafi