Jiji la Dodoma lapongezwa kukusanya zaidi ya 100% mapato ya ndani Mwaka wa Fedha 2025/2026

Na. Leah Mabalwe, DODOMA

Halmashauri ya Jiji la Dodoma yapongezwa kwa namna inavyosimamia na kukusanya mapato, hatua inayochangia kwa kiasi kikubwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika jiji hilo kufuatia ukusanyaji wa zaidi ya asilimia 100 kwa bajeti ya mwaka 2025/2026.



Pongezi hizo zilitolewa na Mbunge wa Viti Maalum, Aisha Msantu mara baada ya kusomwa kwa taarifa ya tathmini ya mapato kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026, katika Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma lililofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo.

Alisema kuwa juhudi zinazoendelea kufanywa na halmashauri katika ukusanyaji na usimamizi wa mapato zinapaswa kupongezwa, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kusimamia vyanzo vya mapato kwa ufanisi ili kuwezesha utekelezaji wa bajeti na mipango ya maendeleo ya jiji. “Nipende kuwapongeza halmashauri kwa namna ambavyo wanaendelea kukusanya na kusimamia mapato. Lakini pia katika utekelezaji wa bajeti ya jiji kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026, tunaona juhudi kubwa zinazofanyika hadi kufikia ukusanyaji mapato wa zaidi ya asilimia 100” alisema Msantu.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mnadani, Mgendi Kerenge alisema kuwa ukusanyaji wa mapato unaofanywa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma unaendelea kuleta matokeo chanya kwa wananchi, kwasababu sehemu ya mapato hayo inaonekana kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali katika kata.



“Halmashauri ya Jiji la Dodoma inaendelea kukusanya mapato, lakini kupitia mapato haya ndiyo tunayoona maendeleo katika kata zetu. Shule zinajengwa, hospitali zinajengwa na maendeleo mbalimbali yanafanyika katika kata zetu kupitia mapato haya haya yanayokusanywa, maendeleo yanayoonekana katika maeneo mbalimbali ya jiji yanatokana kwa kiasi kikubwa na mapato yanayokusanywa na halmashauri, ambayo huwezesha utekelezaji wa miradi muhimu ya kijamii na kiuchumi” alisema Kerenge.

Alisema kuwa ni muhimu wananchi kuendelea kushirikiana na halmashauri katika kuhakikisha wanatimiza wajibu wao wa kulipa kodi na tozo mbalimbali kwa wakati, kwa kuwa mapato hayo ndiyo msingi wa utekelezaji wa huduma na miradi ya maendeleo inayowagusa wananchi moja kwa moja.

Kwa ujumla, viongozi hao wameeleza kuwa kuimarika kwa ukusanyaji na usimamizi wa mapato ni hatua muhimu katika kuhakikisha Halmashauri ya Jiji la Dodoma inaendelea kutekeleza mipango yake ya maendeleo na kuboresha huduma kwa wananchi.

Comments

Popular Posts

Kata ya Miyuji Yaongeza Kasi ya Usimamizi Wa Usafi wa Mazingira

Kata za Nkuhungu na Kizota zajiandaa kukabiliana na mvua za El Nino

Mwenyekiti Mtaa wa Karume, Kata ya Mnadani ahamasisha usafi