Kliniki ya Kata ya Kikuyu Kaskazini kuwasogezea huduma wananchi mlangoni

Na. Leah Mabalwe, DODOMA

Wananchi wa Kata ya Kikuyu Kaskazini Jijini Dodoma wanatarajiwa kunufaika na huduma mbalimbali za serikali kupitia Kliniki ya Kata itakayoanzishwa wiki hii ikiwa ni hatua ya kusogeza huduma karibu na wananchi na kuwawezesha kupata huduma mbalimbali kwa urahisi.



Hayo aliyazungumza Diwani wa Kata ya Kikuyu Kaskazini, Herry Beji nje ya ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Alisema kuwa Kliniki hiyo itafanyika kwa muda wa wiki moja katika Shule ya Msingi Kikuyu, ambapo idara na taasisi mbalimbali zitashiriki katika kutoa huduma kwa wananchi, miongoni mwa huduma zitakazopatikana ni huduma za ardhi. “Lengo letu ni kusogeza huduma karibu na wananchi ili wasipate usumbufu wa kwenda katika ofisi mbalimbali kutafuta huduma, ambapo wataalamu kutoka seksheni ya Ardhi ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma pamoja na Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Dodoma watakuwepo kusikiliza na kushughulikia changamoto mbalimbali za wananchi zinazohusu masuala ya Ardhi  na taasisi nyingine moja kwa moja katika Kata ya Kikuyu Kaskazini” alisema Beji.

Diwani huyo alizitaja huduma nyingine zitakazotolewa kutoka taasisi za DUWASA, TANESCO, Idara ya Afya, NIDA pamoja na taasisi nyingine, ambazo zitapata fursa ya kutoa huduma na kusikiliza changamoto za wananchi katika eneo moja.

Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalum, Aisha Msantu, aliwataka madiwani kuendelea kuwa karibu na wananchi na kusimamia mahitaji pamoja na changamoto zinazowakabili katika maeneo yao ili kuhakikisha yanapatiwa ufumbuzi kwa wakati. “Ni muhimu kuendelea kusikiliza kero za wananchi, ninawasihi madiwani muendelee kuwa karibu na wananchi, msikilize mahitaji yao na muendelee kuyasimamia mpaka yapate majibu. Mwananchi anahitaji kuona kiongozi wake yupo pamoja naye na anasimamia changamoto zinazomkabili” alisema Msantu.

Kliniki ya Kata ni fursa muhimu kwa wananchi kupata huduma mbalimbali kwa wakati mmoja, hivyo wananchi wote wa Kata ya Kikuyu Kaskazini kujitokeza kwa wingi katika Shule ya Msingi Kikuyu ili kupata huduma, ushauri na ufumbuzi wa changamoto zao kutoka kwa taasisi na idara mbalimbali zitakazoshiriki.

Comments

Popular Posts

Kata ya Miyuji Yaongeza Kasi ya Usimamizi Wa Usafi wa Mazingira

Kata za Nkuhungu na Kizota zajiandaa kukabiliana na mvua za El Nino

Mwenyekiti Mtaa wa Karume, Kata ya Mnadani ahamasisha usafi