Kata ya Miyuji Yaongeza Kasi ya Usimamizi Wa Usafi wa Mazingira
Na. Manase Malima, MIYUJI
Kata ya Miyuji katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma
imechukua hatua za kuimarisha usafi wa mazingira kwa kufanya ukaguzi wa vikundi
vinavyohusika na ukusanyaji na uondoshaji wa taka, ikiwa ni sehemu ya
utekelezaji wa wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia
Suluhu Hassan wa kuhakikisha miji na majiji yanakuwa safi.
Katika kutekeleza wito huo, wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kuhakikisha miji na majiji yanakuwa safi, Kata ya Miyuji katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeelekeza nguvu katika kuboresha mfumo wa ukusanyaji na uondoshaji wa taka kupitia vikundi vinavyofanya shughuli hiyo katika mitaa ya kata.
Leo tarehe 11 Septemba, 2026 Kamati ya Maendeleo ya
Kata ya Miyuji, ikiongozwa na Diwani wa Kata hiyo, Ringo Iringo, imefanya
ukaguzi wa vifaa vinavyotumika katika shughuli za usafi, ikiwemo magari, na
vifaa kinga kwa watendaji. Ukaguzi huo umehusisha kuangalia hali ya vifaa,
mahitaji ya vikundi pamoja na uwezo wao wa kutekeleza shughuli za usafi kwa
kuzingatia matakwa ya mikataba yao.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo kwa niaba ya Kamati ya
Maendeleo ya Kata ya Miyuji, Diwani wa kata hiyo, alisema kuwa ukaguzi huo
unalenga kuhakikisha vikundi vinavyohusika na uondoshaji wa taka katika mitaa
vinakuwa na vifaa vinavyokidhi mahitaji na vina uwezo wa kutoa huduma kwa
ufanisi.
Meneja wa Kanda namba Sita, Lucas Venance alisema kuwa ushiriki wao umelenga kushuhudia hatua zinazochukuliwa katika kuboresha huduma za usafi na kuhakikisha vikundi vinakuwa na uwezo na vifaa stahiki kwa ajili ya zoezi la kuondosha taka.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kikundi cha Wanaharakati Mazingira,
Onesmo Mduda ambaye pia ni mkazi wa Kata ya Miyuji alisema kuwa ukaguzi huo ni
muhimu katika kuhakikisha huduma ya ukusanyaji na uondoshaji wa taka inaimarika
na mazingira ya kata yanakuwa safi kwausimamizi mzuri wa vikundi
vinavyotambulika na serikali.
Nae Nasibu Mkuyu ambaye ni mkazi wa Kata ya Miyuji
alisema kuwa usafi wa mazingira unahitaji ushirikiano kati ya viongozi, vikundi
vinavyohusika na uondoshaji wa taka na wananchi, huku akiwataka wananchi
kuzingatia utaratibu wa utunzaji na uondoshaji wa taka.
Zoezi hilo limefanyika kwa ushirikiano na viongozi kutoka Kanda Namba Sita, wakiongozwa na Meneja wa Kanda, pamoja na wataalamu wake. Hatua hiyo inaonesha namna Kata ya Miyuji inavyotekeleza kwa vitendo wito wa Rais wa kuimarisha usafi katika miji na majiji.
Comments
Post a Comment