Kata za Nkuhungu na Kizota zajiandaa kukabiliana na mvua za El Nino
Na. Mwandishi wetu, DODOMA
Kanda
Namba Tatu ya utoaji huduma katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma imefanya zoezi
la usafi wa maeneo ya Kizota Relini na Mkonongo, Kata ya Nkuhungu, ikiwa ni
sehemu ya maandalizi ya kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua
kubwa za El Niño.
Zoezi hilo lilihusisha ufunguaji na usafishaji wa mitaro, uondoaji wa taka pamoja na ukaguzi wa miundombinu ya kupitisha maji, hatua zinazolenga kupunguza hatari ya maji kujaa katika maeneo ya makazi na biashara.
Kaimu
Meneja wa Kanda Namba Tatu, Vestina Manota aliwashukuru watumishi na wananchi
kwa kushiriki katika zoezi hilo, akisema usafi wa mazingira ni muhimu katika
maandalizi ya kukabiliana na athari za mvua za El Niño.
“Tunawahimiza
wananchi kuendelea kufanya usafi kila siku na kuondoa taka kwenye mitaro ili kuhakikisha
maji yanapata njia ya kupita kwa urahisi,” alisema Manota.
Diwani wa Kata ya Nkuhungu, Julius Ezekiel aliwataka wananchi kuchukua tahadhari mapema kwa kufuatilia taarifa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kuhusu mwenendo wa mvua, pamoja na kuendelea kufanya usafi wa maeneo yao kila siku.
Nae
Afisa Afya katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Consolata Urio alisema kuwa usafi
husaidia kuzuia maji kutuama, kuzaliana kwa mbu na kuenea kwa magonjwa, hivyo
aliwataka wananchi kuhakikisha maeneo yao ya makazi na biashara yanakuwa safi
wakati wote.
Kwa
upande wake Ally Salim alisema zoezi hilo limeimarisha umoja na mshikamano
katika kukabiliana na athari za mvua, huku halmashauri ikiwasisitiza wananchi
kuendelea kufanya usafi kila siku, kutunza mitaro na kuepuka kutupa taka kwenye
njia za maji.
Comments
Post a Comment