Zoezi la Kuua Mbwa Wanao Zurura Lafanyika Kata ya Msalato
Na. Manase Malima, MSALATO
Zoezi la kuua mbwa wanao zurura limefanyika katika
Kata ya Msalato, Halmashauri ya Jiji la Dodoma, likihusisha maeneo ya
Machinjioni, Magereza na Mnadani, kutokana na kero na hatari zinazowakabili
wananchi ambapo mbwa zaidi ya 20 waliuliwa.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Afisa Mifugo wa Kanda Namba Sita ya utoaji huduma Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prisca Mottee alisema kuwa mbwa hao wamekuwa wakisababisha usumbufu kwa wananchi, wakiwemo watoto na wanafunzi wanaokwenda na kurudi shuleni, Afisa Mifugo kanda Namba Sita aliongeza kuwa zoezi hilo ni endelevu na litafanyika katika maeneo mengine yenye changamoto hiyo, huku akiwataka wafugaji kuwafungia mbwa wao na kuzingatia kuwapatia chanjo.
Kwa upande wake Afisa Mifugo Kata ya Msalato, Maisha
Jiwa alisema kuwa hatua hiyo imechukuliwa kufuatia malalamiko ya wananchi
kuhusu mbwa wanao zurura katika maeneo mbalimbali ya kata hiyo.
“Kumekuwa na adha kubwa ya mbwa wanaozurura katika maeneo
ya Machinjioni, Mnadani na kwenye makazi ya wananchi. Wanafunzi wamekuwa
wakitishwa na kufukuzwa wanapokwenda au kurudi shule, huku baadhi ya wananchi,
wakiwemo watoto, wakiripotiwa kung’atwa na mbwa hao. Kwa hiyo tumeanza kuchukua
hatua ya kuwaondoa na zoezi hili litaendelea katika maeneo yote yenye
changamoto,” alisema Jiwa.
Jiwa alisisitiza kuwa zoezi hilo pia limehusisha
maeneo ambayo wananchi walitoa taarifa kuhusu usumbufu unaosababishwa na mbwa
wazururaji, ikiwemo eneo la Magereza. Alisema kuwa hatua hiyo inalenga
kupunguza hatari na kurejesha usalama wa wananchi, hasa watoto wanaotumia njia
hizo wakati wa kwenda na kurudi shuleni.
Kwa upande wake, mkazi wa Kata ya Msalato, Godfrey
David, alisema kuwa zoezi hilo ni muhimu kwa kuwa mbwa hao wamekuwa
wakisababisha usumbufu kwa wanafunzi na wananchi, hasa wakati wa asubuhi na
katika eneo la Mnadani. Amesema serikali kuchukua hatua hiyo ni jambo zuri na
amewataka wafugaji kuhakikisha wanawafunga mbwa wao na kuhakikisha hawazururi
mitaani.
Zoezi hilo ni sehemu ya hatua zinazoendelea
kuchukuliwa katika Kata ya Msalato kukabiliana na mbwa wazururaji na kupunguza
madhara kwa wananchi. Wafugaji wa mbwa wametakiwa kuwafungia, kuwapatia chanjo
na kuhakikisha wanawafuga kwa kuzingatia usalama wa jamii.
Comments
Post a Comment