Jiji la Dodoma laimarisha huduma za afya, vituo vyafikia 163

Na. Mwandishi wetu, DODOMA

 

Huduma za afya katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma zimeendelea kuimarishwa, huku vituo vikifikia 163 na watumishi wa afya wakiongezeka hadi 950 mwaka 2025/2026, kutoka 885 mwaka 2024/2025, hatua inayoongeza upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

 


Hayo yameelezwa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Vincent Odero wakati akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 katika mkutano wa Mwaka wa Baraza la Madiwani, ambapo madiwani walipokea taarifa hiyo.

 

Alisema kuwa jiji limeendelea kuimarisha huduma za afya kupitia vituo vya serikali, mashirika ya dini, umma na binafsi, huku idadi ya watumishi ikiongezeka kutoka 885 hadi 950 kati ya mwaka 2024/2025 na 2025/2026.

 

“Jiji la Dodoma lina jumla ya vituo vya kutoa huduma za afya 163, hospitali zikiwa tisa, kati ya hizo hospitali tano ni za serikali, mbili ni za watu binafsi na mbili ni za mashirika ya dini. Vituo vya afya vipo 15, kati ya hivyo, tisa ni vya serikali, kimoja ni cha shirika la dini, vitatu ni vya mashirika ya umma na viwili ni vya watu binafsi,” alisema Odero.

 

“Kuna jumla ya zahanati 99, zahanati za serikali ni 41, zahanati 11 ni za mashirika ya dini, vituo nane ni vya mashirika ya umma na zahanati 40 ni za watu binafsi. Jumla ya kliniki (Polyclinic) ziko 38, zote zikiwa za watu binafsi, na pia kuna kituo kimoja cha binafsi cha kufanya uchunguzi (Diagnostic Centre),” alisema Odero.

 

Aidha, Aliongeza kuwa mfumo wa GOTHOMIS umeendelea kufungwa katika vituo vya afya, ambapo Mwaka 2024/2025 uliwekwa katika vituo vya afya saba na zahanati 41, huku Mwaka 2025/2026 ukiwekwa katika hospitali moja, vituo vya afya tisa na zahanati 44.

 

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Nala, Leonard Malima aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha za kuwajengea Hospitali ya Jiji la Dodoma, akisema imekuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa kata hiyo na maeneo jirani.

 


“Tangu hospitali ya Jiji ilipofunguliwa mpaka sasa, wananchi wa Kata ya Nala na kata za pembezoni wamekuwa wanufaika wakubwa sana wa hii hospitali. Kupitia hospitali hii, wananchi wameendelea kupata huduma za afya kwa urahisi na kwa ukaribu zaidi,” alisema Malima.

 

Hutua hizo zinaendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wa Jiji la Dodoma, hususan katika maeneo ya pembezoni, huku uwepo wa Hospitali ya Jiji la Dodoma ukichochea maendeleo ya huduma na ustawi wa wananchi.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Kata ya Miyuji Yaongeza Kasi ya Usimamizi Wa Usafi wa Mazingira

Kata za Nkuhungu na Kizota zajiandaa kukabiliana na mvua za El Nino

Mwenyekiti Mtaa wa Karume, Kata ya Mnadani ahamasisha usafi