Wakulima wahimizwa kupanda Marigold kufukuza wadudu shambani
Na. Mwandishi wetu, NZUGUNI
Wakulima wa vipando
bustani katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kutumia maua aina ya Marigold
kama njia ya asili ya kudhibiti wadudu na kuboresha mazingira ya mashamba,
hatua inayolenga kupunguza matumizi ya dawa za viwandani katika kilimo.
Ua aina ya Marigold
Akizungumza katika
maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Dkt. John Malecela Afisa
Kilimo wa jiji hilo, Fatuma Doow alisema kuwa matumizi sahihi ya maua ya Marigold
ni sehemu muhimu ya kuboresha afya ya mashamba na bustani kwa kuongeza thamani
ya mandhari ya maeneo ya kilimo.
Alisema kuwa maua ya Marigold
yanapandwa pembezoni mwa vipando vya bustani na husaidia kuongeza urembo,
sambamba na kusaidia kuzuia na kufukuza baadhi ya wadudu wanaoweza kuhamia
kutoka katika mashamba mengine.
“Ushauri wangu kwa
wakulima wa mazao ya bustani ni kupanda maua pembezoni mwa mazao hayo ili
kusaidia kupunguza matumizi ya dawa za wadudu na kuimarisha matumizi ya njia rafiki
kwa mazingira katika udhibiti wa wadudu,” alisema Doow.
Kwa upande wake, mdau na
mfanyabiashara wa Maua katika Jiji la Dodoma, Monica Mhina alisema kuwa sekta
ya maua ina fursa kubwa kutokana na kuongezeka kwa uelewa wa wananchi kuhusu
umuhimu wa mimea ya mapambo katika kuboresha mazingira na maisha ya kila siku.
“Kuna maua ya aina
mbalimbali yenye faida tofauti, lakini Ulimi wa mama mkwe husaidia kuboresha
hewa ndani ya nyumba, Saigonia hupendezesha mazingira na husaidia kupunguza
mawazo. Pia, watu wengi hupenda ‘money tree’ kutokana na imani kwamba huleta
mafanikio na ustawi. Ninawashauri wananchi wenzangu kupanda maua kwa sababu
yana faida nyingi zaidi ya urembo,” alisema Mhina.
Nae, mkazi wa Jiji la
Dodoma aliyefika kutembelea maonesho hayo kwa ajili ya kujifunza, Asha
Mwakalobo alisema kuwa amepata maarifa mapya kuhusu umuhimu wa maua katika
maisha ya kila siku.
“Nilikuwa najua maua ni
kwa ajili ya urembo tu, lakini leo nimejifunza kwamba mengine yanaweza kusaidia
kupunguza wadudu mashambani na kuboresha hewa ndani ya nyumba. Nimepata hamasa
ya kuanzisha bustani ndogo nyumbani kwangu,” alisema Mwakalobo.
Ua aina ya Saigonia husaidia kuondoa stress
Maonesho ya Nanenane yameendelea kuwa jukwaa la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu teknolojia, ubunifu na mbinu mbalimbali za kuboresha uzalishaji wa kilimo pamoja na utunzaji wa mazingira.
Comments
Post a Comment