Silage suluhisho la uhaba wa chakula cha mifugo Dodoma
Na. Mwandishi wetu, NZUGUNI
Wafugaji wa ng’ombe katika
Halmashauri ya Jiji la Dodoma wamehimizwa kuanza kutengeneza na kuhifadhi
chakula cha mifugo kilichochachushwa (Silage) ili kuhakikisha mifugo inapata
lishe ya kutosha wakati wa kiangazi, kipindi ambacho maeneo mengi hukumbwa na
upungufu mkubwa wa malisho kutokana na ukame.
Rai hiyo ilitolewa na Afisa Mifugo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Delila Mlamka wakati akiwaelezea wananchi waliotembelea banda la mifugo la halmashauri hiyo katika maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini hapa.
Alisema kuwa Silage ni chakula
kinachotengenezwa kwa kuchanganya majani mabichi yaliyokatwakatwa, kiasi kidogo
cha majani makavu, pumba na molases, kisha kuhifadhiwa kwenye mazingira
yasiyoruhusu hewa ya oksijeni kuingia kwa siku 21 ili kichachuke vizuri na kuwa
salama kwa matumizi ya mifugo.
Alisema kuwa chakula hicho kinaweza kutengenezwa kwenye mashimo au
mapipa na kuhifadhiwa katika mifuko midogo ya plastiki na mifuko maalumu ya
kuhifadhia nafaka ‘kinga njaa’, ila tu hewa isiingie ndani ya kifungashio.
“Silage ni lishe bora na kinapendwa
sana na ng’ombe wa maziwa kwa sababu kina mchanganyiko wa majani, pumba na
molases unaosaidia kuongeza virutubisho muhimu kwa ukuaji wa mifugo na
uzalishaji wa maziwa. Chakula hiki kinaweza kuhifadhiwa kwa zaidi ya miaka
miwili bila kuharibika endapo kitaandaliwa na kuhifadhiwa kwa usahihi,” alisema
Mlamka.
Kwa upande wake mfugaji wa ng’ombe
kutoka Kata ya Nzuguni, Mussa Elisha alisema kuwa teknolojia ya silage itakuwa
msaada mkubwa kwa wafugaji, hasa wakati wa kiangazi ambapo malisho hupungua kwa
kiasi kikubwa.
“Hapo zamani tulipata wakati mgumu
kulisha mifugo kipindi cha ukame, lakini sasa tukitengeneza silage mapema
tunakuwa na uhakika wa chakula kwa muda mrefu. Hii itachangia mifugo yetu
kubaki na afya nzuri na uzalishaji wa maziwa kuendelea hata wakati wa
kiangazi,” alisema Elisha.
Kwa upande wake mdau wa mifugo katika
Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Elineema Kikumbi alisema kuwa utunzaji wa
malisho kupitia teknolojia ya silage ni hatua muhimu ya kuongeza tija katika
sekta ya mifugo na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Dodoma ni moja ya maeneo
yanayokumbwa na ukame mara kwa mara. Wafugaji wanapaswa kutumia kipindi cha
mvua kuandaa akiba ya chakula cha mifugo. Silage ni suluhisho la kudumu ambalo
litasaidia kupunguza vifo vya mifugo, kuongeza uzalishaji na kuinua kipato cha
wafugaji,” alisema Kikumbi.
Wataalamu wa mifugo wanaendelea
kuhimiza wafugaji kuwekeza katika utengenezaji wa silage ili kuwa na akiba ya
malisho mwaka mzima, hatua itakayosaidia kuongeza uzalishaji wa maziwa na nyama
pamoja na kuimarisha ustahimilivu wa sekta ya mifugo dhidi ya ukame.
Comments
Post a Comment