Matenga yageuka lulu kilimo cha mbogamboga Dodoma
Na. Mwandishi wetu, NZUGUNI
Wananchi wanaoishi mijini,
hususan kwenye nyumba za kupanga wametakiwa kutumia matenga, makopo ya maji na
matairi yaliyotumika kuanzisha bustani za mbogamboga majumbani ili
kujihakikishia upatikanaji wa chakula salama, kupunguza gharama za maisha na
kuhifadhi mazingira.
Wito huo ulitolewa na Afisa Kilimo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Zaidina Juma wakati wa maonesho ya 32 ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Malecela mjini Dodoma.
Alisema kuwa kilimo cha
kwenye matenga ni njia rahisi inayosaidia kuhifadhi mazingira huku kikitatua
changamoto ya upatikanaji wa maeneo ya kulima.
Alisema kuwa wananchi
wengi wanaishi kwenye nyumba za kupanga au maghorofani ambako hakuna nafasi ya
kuanzisha bustani za kawaida, lakini bado wanaweza kuzalisha mboga zao kwa
kutumia vifaa vinavyotupwa na kula mboga zenye usalama, tofauti na baadhi ya
mazao yanayouzwa sokoni ambayo wakati mwingine huvunwa muda mfupi baada ya
kunyunyiziwa viuatilifu.
“Ukilima nyumbani unakuwa na uhakika wa kile
unachokula, kwa sababu unajua namna ulivyokizalisha na huna wasiwasi wa
kemikali zinazoweza kubaki kwenye mboga. Badala ya kutupa makopo, matairi au
matenga, vitumike kuzalisha chakula. Hii ni njia ya kuhifadhi mazingira na
wakati huohuo, kuongeza usalama wa chakula kwenye kaya,” alisema Juma.
Kwa upande wake Mdau wa
Kilimo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Juma Mtega alisema kuwa bustani za
kwenye matenga ni suluhisho linalokwenda sambamba na ukuaji wa miji, kwasababu zinawawezesha
wananchi kuzalisha chakula hata katika maeneo yenye nafasi ndogo.
“Leo watu wengi wanaishi
kwenye nyumba za kupanga na viwanja vidogo. Teknolojia hii inawapa fursa ya
kujitosheleza kwa mboga, kupunguza matumizi ya fedha na kuongeza lishe kwa
familia,” alisema Mtega.
Nae, mkazi wa Kata ya
Chang’ombe Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Asha Hamis anayeishi katika nyumba ya
kupanga alisema kuwa maonesho hayo yamempa hamasa na fursa ya kujifunza kilimo cha
mjini ambacho hakina gharama kubwa katika kukianzisha.
“Nimeona kumbe si lazima
uwe na shamba. Nikipata matenga mawili au matatu na kupanda mboga zangu,
nitapunguza gharama za kununua mboga kila siku na nitakuwa na uhakika wa ubora
wake,” alisema Hamis.
Comments
Post a Comment