Dodoma yazalisha Bayogesi kulinda utunzaji wa Mazingira na matumizi ya Nishati safi
Na. Mwandishi wetu, DODOMA
Halmashauri ya Jiji la Dodoma
imeendelea kuonesha dhamira yake ya kulinda mazingira kwa kuhamasisha matumizi
ya nishati safi kupitia uzalishaji wa bayogesi (Biogas) inayotokana na kinyesi
cha mifugo na mabaki ya chakula ikiwa ni kuunga mkono za Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania za kuhimiza matumizi ya nishati safi, uhifadhi wa
mazingira na maendeleo endelevu.
Akizungumza katika Maonesho ya
Kitaifa ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Malecela,
Nzuguni jijini Dodoma, Daktari wa Mifugo kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma,
Dkt. Innocent Kimweri alisema kuwa seksheni ya mifugo kimebuni mfumo wa
kuzalisha bayogesi kwa kutumia kinyesi cha mifugo na mabaki ya chakula. Alisema
kuwa ubunifu huo unalenga kupunguza uchafuzi wa mazingira, kuboresha usimamizi
wa taka na kuongeza matumizi ya nishati mbadala.
Akifafanua zaidi, alisema kuwa mfumo
huo unahusisha kuchakata kinyesi cha mifugo na mabaki ya chakula kwa kuyapeleka
kwenye mtambo maalumu unaozalisha bayogesi. Aliongeza kuwa nishati hiyo
hutumika kwa shughuli mbalimbali ikiwemo kupikia, wakati joto linalozalishwa
likitumika kuwahifadhi na kuwapa joto wanyama wadogo wanaozaliwa. Aidha,
teknolojia hiyo husaidia kupunguza harufu mbaya, uchafuzi wa mazingira na
gharama za matumizi ya nishati.
Dkt. Kimweri aliwahimiza wananchi,
kujifunza na kutumia teknolojia hiyo katika maeneo yao ili kuboresha usimamizi
wa taka, kulinda mazingira, kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza
matumizi ya nishati safi. Aliongeza kuwa matumizi ya bayogesi pia yanasaidia
kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, hatua inayochangia katika uhifadhi wa
misitu na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma
inaendelea kutoa elimu na kuonesha teknolojia mbalimbali za kisasa katika sekta
za kilimo, mifugo na uvuvi kupitia banda lake katika Maonesho ya Kitaifa ya
Nanenane, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha matumizi ya teknolojia
rafiki kwa mazingira na kuongeza tija katika uzalishaji.
MWISHO
Comments
Post a Comment