Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Wilaya ya Dodoma lapata viongozi wapya kwa miaka mitatu
Na. Mwandishi wetu, VIWANDANI
Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Wilaya ya
Dodoma limepata uongozi mpya utakaohudumu kwa kipindi cha miaka mitatu baada ya
uchaguzi uliofanyika kwa ushindani mkubwa.
Zoezi hilo limefanyika katika Viwanja vya Nyerere Square, Kata ya Viwandani, jijini Dodoma kwa lengo la kupata uongozi mpya wa ngazi ya wilaya kwa nafasi za mwenyekiti, makamu mwenyekiti, katibu, katibu msaidizi na wawakilishi.
Bhoke Manyori alichaguliwa kuwa Mwenyekiti baada ya
kupata kura 54 dhidi ya Elizabeth Kasimila aliyepata kura 50 na kuchaguliwa
kuwa Makamu Mwenyekiti.
Nafasi ya Katibu ilichukuliwa na Fatuma Saidi
aliyepata kura 82, akifuatiwa na Janeth Bubegwa aliyepata kura 27, huku Joyce
Masi akipata kura 13, ambapo Bubegwa akichaguliwa kuwa Katibu Msaidizi.
Katika nafasi ya uwakilishi, Ashura Nguya na Joyce
Masi walipitishwa bila kupingwa na kuwa wawakilishi wa Jukwaa la Uwezeshaji
Wanawake Kiuchumi Wilaya ya Dodoma.
Akizungumza baada ya kuchaguliwa, Mwenyekiti wa Jukwaa
hilo, Bhoke Manyori aliwashukuru wajumbe kwa kumuamini na kuomba ushirikiano
katika kutekeleza majukumu ya jukwaa.
“Dhamana hii nimepewa na wajumbe, hivyo nawaomba
tushirikiane kwa karibu ili tuweze kusukuma mbele shughuli za jukwaa na kuleta
matokeo yanayolenga kuwawezesha wanawake,” alisema Manyori.
Kwa upande wake, Katibu wa Jukwaa hilo, Fatuma Saidi
alisema kuwa nafasi hizo ni za kujitolea na zinahitaji viongozi kutenga muda
kwa ajili ya majukumu ya jukwaa huku wakiendelea na shughuli zao za kiuchumi.
“Kwa kura hizi mlizonikopesha mnatamani mfike pale
ambapo mnatamani kufika. Kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu na kwa msaada wake na
kushirikiana na viongozi wenzetu, tutafika kule ambapo tunatamani tufike,”
alisema Saidi.
Nae, Mwakilishi wa Jukwaa hilo, Ashura Nguya aliwaomba
viongozi waliochaguliwa kutembelea kata mbalimbali na kuzungumza na wanawake
ili wawakilishi waweze kukusanya taarifa kuhusu mahitaji na changamoto zao na
kuzifikisha katika ngazi husika.
Uzinduzi wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi
Wilaya ya Dodoma umefanyika chini ya kaulimbiu isemayo “Agenda 2050: Familia
Imara, Jamii Imara, Taifa Imara.” na limezinduliwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Alhaj
Jabir Shekimweri.
Comments
Post a Comment