Jukwaa la Wanawake kiuchumi laweka nguvu ngazi ya Mtaa

Na. Mwandishi wetu, VIWANDANI

 

Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Wilaya ya Dodoma limeweka mkazo katika ngazi ya mtaa, likilenga kuimarisha usimamizi wa miradi, fedha na shughuli za kiuchumi za vikundi.

 


Hayo yameelezwa wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Wilaya ya Dodoma, uliofanyika katika Viwanja vya Nyerere Square, Kata ya Viwandani, Jiji la Dodoma.

 

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mratibu wa jukwaa hilo Wilaya ya Dodoma, Theresia Camilius alisema kuwa mfumo huo huanzia kwenye vikundi vya ujasiriamali vinavyosajiliwa na kutambuliwa, kisha kuunda jukwaa la mtaa.

 

Alisema kuwa majukwaa hayo yanajumuisha wanachama kutoka vikundi vya ujasiriamali, biashara, miradi pamoja na huduma ndogo za fedha kama VIKOBA, hivyo kuwaunganisha katika mfumo mmoja wa kusimamia shughuli zao za kiuchumi.

 

“Wanawake wanaungana, wakishaungana na kuunda jukwaa la mtaa, wanampata mwenyekiti, makamu mwenyekiti, wanampata katibu, katibu msaidizi, lakini pia na mweka hazina,” alisema Camilius.

 

Aliongeza kuwa kila jukwaa la mtaa huchagua wawakilishi watano wanaounda jukwaa la kata pamoja na wenzao kutoka mitaa mingine, ambapo huchaguliwa viongozi na wawakilishi watatu wa kwenda ngazi ya wilaya.

 

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa jukwaa hilo, Elizabeth Kasimila alisema kuwa ushirikiano wa viongozi ni muhimu katika kuwaunganisha wanachama na fursa za kiuchumi.

 

“Ninajua kutafuta fursa za wanawake, ninajua kupita chocho za kupata fursa za kiuchumi, lakini kwa kushirikiana na Bhoke tutaweza kuzitafuta na kuwasaidia wanawake,” alisema Kasimila.

 

Nae, Katibu Msaidizi wa Jukwaa hilo, Janeth Bubegwa alisema kuwa ushirikiano wa viongozi wa serikali na watendaji wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii utasaidia kufikia malengo yaliyowekwa.

 

“Tumekuwa tukifanywa daraja na wanawake wa mikoa mingine wakati sisi tuko makao makuu. Ninaamini kwa ushirikiano wa viongozi wetu wa serikali, tutayafikia malengo ambayo tumeyakusudia,” alisema Bubegwa.

 

Jukwaa hilo linatarajiwa kuimarisha ushiriki wa wanawake katika shughuli za kiuchumi kwa kuwaweka katika mtandao unaorahisisha usimamizi wa vikundi, miradi na upatikanaji wa fursa katika ngazi za chini.




Comments

Popular Posts

Jiji la Dodoma Biashara saa 24, usafi saa 24

Mvua za El Nino: DC Shekimweri awaasa wananchi wa Dodoma Kuchukua Tahadhari

Wananchi Dodoma wahimizwa kufanya usafi wa Mazingira kila siku