Eneo lililoathiriwa na moto Soko la Machinga kurejea ndani ya siku 10
Na. Mwandishi wetu, DODOMA
Soko la wazi la Machinga lililoathiriwa
na moto mkubwa uliotokea tarehe 20 Septemba, 2026 linatarajiwa kurejea katika
hali ya kawaida ndani ya siku 10, huku Halmashauri ya Jiji la Dodoma likianza
kuchukua hatua za kurekebisha maeneo yaliyoathirika na kuboresha mpangilio wa
biashara.
Hayo yalisemwa na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Alimwoni Chaula baada ya kutembelea soko hilo kwa lengo la kukagua madhara yaliyosababishwa na moto huo na kutoa pole kwa wafanyabiashara wa soko hilo.
“Leo tumekuja kujionea madhara
waliyopata wafanyabiashara wetu wa machinga ambapo juzi ulitokea moto mkubwa
ambao uliathiri vibanda mbalimbali vya wafanyabiashara wa Dodoma. Pia nitoe
pongezi kwa uongozi wa mkoa na wilaya, Jeshi la Polisi pamoja na Jeshi la
Zimamoto na Uokoaji kwa kusaidia kuzuia moto huo kusababisha madhara makubwa
zaidi,” alisema Chaula.
Alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la
Dodoma inatekeleza maelekezo ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kuhakikisha
wafanyabiashara walioathirika wanarejea katika shughuli zao ndani ya siku 10,
huku hatua zikichukuliwa kuboresha usalama wa soko hilo.
Alisema kuwa uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma unafanya mapitio ya mpangilio wa biashara, ikiwemo kuhakikisha njia za magari ya zimamoto zinaachwa wazi na kupunguza msongamano wa bidhaa. Pia aliwataka wafanyabiashara wenye mitaji mikubwa kuachia nafasi kwa wafanyabiashara wadogo na wanaoanza biashara.
Comments
Post a Comment