DC Shekimweri asisitiza urasimishaji biashara za wanawake
Na. Paulo Paulo, VIWANDANI
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir
Shekimweri ametoa rai kwa wanawake wajasiriamali kutumia vema fursa ya uwepo wa
Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi ili kukuza biashara zao na kuchangia
katika maendeleo ya uchumi wa taifa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Wilaya ya Dodoma, aliwapongeza viongozi wapya waliochaguliwa na kuwataka kutekeleza majukumu yao kwa tija, uadilifu na ushirikiano mkubwa na serikali pamoja na mamlaka husika.
Sambamba na hilo aliwataka wajasiriamali kurasimisha
biashara zao ili kuongeza fursa za kutambulika, kupata masoko mapya, na
kufaidika na fursa za uwekezaji na mikopo pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
kuendelea kutoa elimu, ushauri, na kujenga mahusiano mazuri na wafanyabiashara
wadogo badala ya kulenga ukusanyaji wa kodi pekee.
Aliwahimiza wanawake kutumia teknolojia ya
kidijitali na mifumo ya kisasa katika kutafuta masoko na kusimamia fedha za
biashara zao. Pia alibainisha kuwa wajasiriamali wadogo ni nguzo muhimu katika
uzalishaji wa ajira na kuimarisha amani na utulivu katika jamii.
Aidha, Alhaj Shekimweri aliwahakikishia
wanawake hao kuwa serikali kupitia ngazi za mkoa, wilaya, na kata itaendelea
kutoa ushirikiano na kuweka mazingira wezeshi ili kuhakikisha malengo ya jukwaa
hilo yanafikiwa.
Comments
Post a Comment