AI Ultrasound kuokoa maisha ya Mama na Mtoto Dodoma

Na. Lulu Luvanda, MKONZE

Mkoa wa Dodoma umechaguliwa kuwa mkoa wa majaribio katika matumizi ya teknolojia ya AI Ultrasound, kupitia Mradi wa The Study of AI-Facilitated Ultrasound Feasibility and Assessment of Resources and Integration (SAFARI Project), unaolenga kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto.



Hatua hiyo imekuja wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa vya AI Ultrasound kwa vituo 32 vya kutolea huduma za afya katika Mkoa wa Dodoma, iliyofanyika katika Kituo cha Afya Mkonze, jijini Dodoma.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, alikipongeza  Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa kuendelea kufanya tafiti zenye uhalisia na zinazolenga kutatua changamoto mbalimbali katika jamii, ikiwemo tafiti katika sekta za Utalii, Mazingira pamoja na Lishe.

Alisema kuwa matumizi ya vifaa hivyo katika vituo vya afya yatawezesha wananchi kupata huduma za awali kwa ukaribu zaidi, hivyo kupunguza changamoto ya kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za uchunguzi wa Ultrasound.



Alishukuru kwa Dodoma kuchaguliwa kuwa mkoa wa majaribio wa matumizi ya teknolojia hiyo, akieleza kuwa uzoefu utakaopatikana unaweza kuwa msingi wa matumizi ya teknolojia hiyo katika mikoa mingine nchini Tanzania.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,  Dkt. Thomas Ruta alisema kuwa AI Ultrasound ni teknolojia yenye uwezo wa kusaidia katika uchunguzi wa mapema na hivyo kuchangia katika kuokoa maisha ya mama na mtoto, hasa watoto wadogo.

Alisisitiza kuwa vifaa hivyo vinapaswa kutumika ipasavyo na wataalamu wa afya, badala ya kuhifadhiwa stoo, huku akihimiza maafisa afya na wauguzi kutumia teknolojia hiyo katika kutoa huduma bora, za karibu na zenye utu kwa wananchi.

Comments

Popular Posts

Kata ya Miyuji Yaongeza Kasi ya Usimamizi Wa Usafi wa Mazingira

Kata za Nkuhungu na Kizota zajiandaa kukabiliana na mvua za El Nino

Mwenyekiti Mtaa wa Karume, Kata ya Mnadani ahamasisha usafi