Wananchi kupatiwa elimu ya fursa za kiuchumi na mikopo ya 7%
Na. Mwandishi wetu, DODOMA
Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeendelea kutoa elimu
kwa wananchi kuhusu fursa mbalimbali za kiuchumi na mikopo inayotolewa kupitia
mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, ikiwa ni sehemu ya shughuli za Mwezi wa
Maendeleo ya Jamii, unaolenga kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi na
kupunguza umaskini.
Akizungumza kuhusu shughuli za uwezeshaji
zinazotekelezwa katika kipindi hicho, Mratibu wa Dawati la Uwezeshaji na
Kupunguza Umaskini, Hidaya Mizega alisema kuwa wananchi wanaendelea kupewa
elimu kuhusu fursa mbalimbali za kiuchumi, namna ya kuzifikia na kuzitumia kwa
ajili ya kuendeleza shughuli zao.
“Elimu hiyo pia inalenga kuwafahamisha wananchi kuhusu
mikopo inayotolewa na halmashauri, ikiwemo mikopo yenye riba ya asilimia saba
kwa wafanyabiashara wadogo maarufu kama machinga, ili kuwawezesha kukuza
biashara zao na kuongeza kipato,” alisema Mizega.
Aliongeza kuwa wananchi wanapaswa kutumia fursa hizo kwa
maendeleo yao, huku akisisitiza umuhimu wa kupata elimu sahihi kuhusu taratibu
na namna ya kunufaika na fursa zinazotolewa kupitia mifuko mbalimbali ya
uwezeshaji.
Halmashauri itaendelea kuwaunganisha wananchi na fursa
mbalimbali za kiuchumi ili kuwasaidia kujenga uwezo wa kujitegemea, kuongeza
kipato na kuchangia katika kupunguza umaskini katika jamii.
Comments
Post a Comment