Jiji la Dodoma laimarisha huduma za Kilimo na Mifugo
Na. Mwandishi wetu, DODOMA
Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wamepokea
taarifa ya utekelezaji wa shughuli za kilimo na mifugo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026,
ikiwemo utoaji wa chanjo, utambuzi na usajili wa mifugo, ukaguzi wa nyama na ‘Agrovet’,
pamoja na udhibiti wa visumbufu vya mazao.
Akizungumza katika Mkutano wa Mwaka wa Baraza la
Madiwani, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Vincent Odero, alisema kuwa
katika Mwaka wa Fedha 2024/2025 na 2025/2026, halmashauri ilitekeleza shughuli
mbalimbali za kilimo na mifugo kwa lengo la kuongeza uzalishaji, kuimarisha
usalama wa chakula na kuboresha huduma kwa wananchi.
Alisema kuwa shughuli hizo zilihusisha utoaji wa
chanjo kwa mifugo, utambuzi na usajili wa mifugo kwa kutumia hereni za
kielektroniki, uhamasishaji wa msimu wa kilimo pamoja na udhibiti wa wadudu na
magonjwa katika mazao ya bustani na zabibu.
“Katika kipindi hiki, tumetekeleza shughuli mbalimbali
za kilimo na mifugo kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na
kuongeza uzalishaji. Hali ya chakula imeimarika kutoka wastani mwaka 2024/2025
hadi kufikia kiwango kizuri Mwaka 2025/2026. Aidha, tumetambua na kusajili
ng’ombe 15,177, mbuzi 5,618 na kondoo 1,015 kwa kutumia hereni za
kielektroniki,” alisema Odero.
Odero aliongeza kuwa ukaguzi wa nyama umeongezeka,
ambapo katika Mwaka 2024/2025 ng’ombe 46,876, mbuzi 63,267, kondoo 3,546 na
kuku 376,213 walikaguliwa, idadi iliyoongezeka katika Mwaka 2025/2026 hadi
kufikia ng’ombe 56,517, mbuzi 67,445, kondoo 3,919 na kuku 415,865, huku ukaguzi
wa maduka ya dawa na pembejeo za mifugo (Agrovet) ukiongezeka kutoka 42 Mwaka
2024/2025 hadi 57 mwaka 2025/2026.
Akichangia taarifa hiyo, Diwani wa Kata ya Matumbulu,
Godfrey Mtizi aliipongeza halmashauri hiyo kwa hatua inazoendelea kuchukua
katika kuimarisha kilimo na ufugaji, akisema wananchi wanahitaji kuendelea
kuona matokeo ya uwekezaji katika sekta hizo.
Alisema kuwa Kata ya Matumbulu ina wakulima na
wafugaji, huku zabibu, mtama na mahindi kiwa miongoni mwa mazao muhimu ya
biashara yanayolimwa katika eneo hilo, ambapo matarajio ya wananchi wanategemea
huduma bora na maendeleo zaidi kutoka katika Jiji la Dodoma.
“Niipongeze Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kazi
kubwa wanayoendelea kuifanya. Tunaamini katika bajeti ya Mwaka 2026/2027
wakulima na wafugaji wataendelea kukumbukwa katika kila sekta. Madiwani
tutaendelea kutoa ushirikiano kwa halmashauri ili kutimiza matarajio ya
wananchi wanayotarajia,” alisema Mtizi.
Utekelezaji wa shughuli hizo unaendelea kuimarisha
sekta za kilimo na mifugo katika Jiji la Dodoma, huku ukilenga kuongeza
uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula na kuboresha maisha ya wananchi,
ambao wanaendelea kutarajia huduma na matokeo zaidi kutoka kwa halmashauri.
MWISHO
Comments
Post a Comment