Mwezi wa Maendeleo ya Jamii kufungua fursa za kiuchumi kwa Vijana Dodoma
Na. Mwandishi wetu, DODOMA
Halmashauri ya Jiji la Dodoma imesema itaendelea
kufungua na kuwawezesha vijana kutumia fursa mbalimbali za kiuchumi na kijamii
kupitia Mwezi wa Maendeleo ya Jamii, kwa lengo la kuwajengea uwezo na
kuwawezesha kujitegemea.
Akizungumza kuhusu shughuli zitakazotekelezwa katika
Mwezi wa Maendeleo ya Jamii, Afisa Vijana wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma,
Joseph Ndulani alisema kuwa moja ya maeneo yatakayopewa kipaumbele ni
kuwawezesha vijana kupata fursa za kiuchumi.
Aliongeza kuwa fursa hizo ni pamoja na mikopo ya
asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa wafanyabiashara
wadogo, maarufu kama machinga.
“Halmashauri pia itaendelea kutoa elimu ya
ujasiriamali na stadi mbalimbali kwa vijana ili kuwajengea uwezo wa kutumia
fursa zinazopatikana na kuendeleza shughuli zao za kiuchumi,” alisema Ndulani.
Aliongeza kuwa Halmashauri itaendelea kutekeleza Sera
ya Maendeleo ya Vijana pamoja na kuwaunganisha vijana na tenda za serikali,
hatua inayolenga kuwapa nafasi ya kushiriki katika shughuli mbalimbali za
kiuchumi.
Vijana wametakiwa kutambua na kutumia fursa
zinazopatikana kwa manufaa yao, huku wakihimizwa kushirikiana na kushiriki
kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya jamii ili kuchangia maendeleo ya
Jiji la Dodoma.
Comments
Post a Comment