Makutupora kupata Zahanati Mpya, Mbunge wa Mtumba aweka nguvu kwenye ujenzi
Na. Mwandishi wetu, MAKUTUPORA
Jitihada za kukamilisha ujenzi wa
Zahanati ya Mchemwa zimepata nguvu baada ya kuchangiwa matofali 5,000, mifuko
250 ya saruji pamoja na gharama za mafundi hadi hatua ya kufunika jengo, huku
wananchi wakihimizwa kushiriki kikamilifu kuhakikisha zahanati hiyo inakamilika
na kuanza kutoa huduma.
Mbunge wa Jimbo la Mtumba Anthony Mavunde alisema kuwa lengo la mchango huo ni kuhakikisha wananchi wa Makutupora wanapata huduma za afya karibu na makazi yao, akisisitiza kuwa ujenzi wa zahanati hiyo haupaswi kuwa jukumu la mtu mmoja, bali ni mradi wa wananchi wote.
“Zahanati si ya kwangu. Zahanati ni ya
kwetu. Kila mmoja ahakikishe pale mchanga wake unaingia kwenye zahanati. Naomba
mtoe ushirikiano. Kuna baadhi ya gharama si lazima nilipie mimi ila nguvu kazi
yenu nayo inaweza kufanikisha jambo hili natamani kuwaona vijana wa hapa
wakichapa kazi,” alisema Mavunde.
Mbunge huyo pia alisema kuwa anaamini serikali
itaendelea kuunga mkono jitihada za wananchi katika ujenzi wa zahanati hiyo,
akieleza kuwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka msisitizo katika kuboresha
huduma za afya, hasa afya ya mama na mtoto.
Akizungumza katika tukio hilo, Mstahiki
Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Alimwoni Chaula ambaye ni Diwani wa Kata
ya Makutupora aliahidi kuunga mkono ujenzi wa zahanati hiyo hadi
utakapokamilika, akisisitiza kuwa zoezi hilo halipaswi kuishia katika siku ya
kukabidhi vifaa vya ujenzi.
“Hii shughuli wananchi si kwamba
inaenda eti inaishia leo kukabidhi. Hapana, tunahitaji ndani ya wiki moja
angalau tuone ukuta umefika eneo gani na kwenye bajeti yoyote nitaunga mkono
mpaka kituo tuwe tumemaliza,” alisema Chaula.
Aidha, alisema kuwa ujenzi wa zahanati
hiyo una umuhimu mkubwa kwa jamii kwa kuwa utasaidia kusogeza huduma za afya
karibu na wananchi na kuokoa maisha ya watu mbalimbali, wakiwemo wanawake na
watoto.
Akizungumza
kwa niaba ya wananchi, mkazi wa Makutupora, Selina Ruben aliwashukuru Mbunge wa
Jimbo la Mtumba, viongozi na wadau wote waliojitokeza kuunga mkono ujenzi wa
zahanati hiyo, akisema kuwa mradi huo umewapa matumaini makubwa ya kupata
huduma za afya karibu na makazi yao.
“Tunawashukuru
sana viongozi wetu kwa hatua hii kubwa. Kwa muda mrefu tumekuwa tukipata
changamoto ya kufuata huduma za afya mbali, hasa mama wajawazito, watoto na
wazee. Kukamilika kwa zahanati hii kutakuwa msaada mkubwa sana kwetu,” alisema.
Comments
Post a Comment