Wafanyabiashara Soko la Miembeni Waazimia Kulinda Usafi
Na. Mohammed Ramadhani, DODOMA
Wafanyabiashara
wa Soko la Miembeni jijini Dodoma wameahidi kuendelea kuimarisha usafi wa
mazingira katika maeneo yao ya biashara, wakieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu
katika kulinda afya na ustawi wa jamii.
Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu wa Soko la Miembeni, Adelgot Mbwani alisema kuwa uongozi wa soko unaendelea kuwahamasisha wafanyabiashara kufanya usafi mara kwa mara na kuhakikisha kila mmoja anawajibika kutunza mazingira yanayomzunguka katika eneo lake la biashara.
Aliongeza
kuwa juhudi hizo pia zinaendana na msisitizo wa serikali wa kuhakikisha miji na
maeneo ya biashara yanakuwa safi, hivyo wafanyabiashara wataendelea kushiriki
kikamilifu katika kampeni za usafi. “Tumekuwa tukiwahamasisha wafanyabiashara
wetu kufanya usafi mara kwa mara na kuwasisitizia kuwa usafi ni jukumu lao
katika maeneo yao ya kazi, kama ambavyo Mheshimiwa Rais anavyosisitiza kuwa majiji
yote yawe safi,” alisema Mbwani.
Kwa
upande wake, Katibu wa Soko la Wauza Chuma, Benson Kihade alisema kuwa kampeni
ya usafi imeanza katika Kanda Namba Moja ikiwa na lengo la kuhakikisha
mazingira ya maeneo yote yanakuwa safi na salama.
Alisisitiza
kuwa zoezi hilo linahusisha kata zote tisa zilizopo katika Kanda Namba Moja
huku viongozi wa mitaa na kata, wenyeviti pamoja na wananchi wakishirikiana
katika utekelezaji wa usafi wa mazingira.
Kihade
alisema kuwa usafi huo hautakuwa wa muda mfupi, bali ni zoezi endelevu la kila
siku litakalosimamiwa na viongozi pamoja na wananchi ili kuhakikisha mazingira
yanabaki safi. “Sisi Kanda Namba Moja ambayo ipo katikati ya mji, kuanzia sasa
tumeanza kampeni ya usafi wa kila siku katika kata zote tisa chini ya usimamizi
wa watendaji wa mitaa, kata, wenyeviti na viongozi wengine wote. Tumeshirikiana
na wananchi kufanya usafi wa mazingira zoezi ambalo litakuwa endelevu kwasababu
tunajua maisha ya mwanadamu ni usafi” alisema.
Aidha,
Kihade alitoa tahadhari kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wafanyaniashara
watakaokiuka taratibu za usafi kwa kutotunza mazingira yao, akieleza kuwa
kuwepo kwa adhabu kutasaidia kuongeza uwajibikaji miongoni mwa wafanyabiashara
na wananchi.
Juhudi
hizo zinaendelea kuhamasisha wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kutambua
kuwa usafi wa masoko na maeneo ya biashara ni sehemu muhimu ya kulinda afya ya
jamii, kuboresha mazingira ya biashara na kuunga mkono azma ya kuwa na miji
safi na salama.
Comments
Post a Comment