LAAC yaridhishwa, yalipongeza Jiji la Dodoma ujenzi wa Barabara ya KM 1.6
Na. Maandishi wetu, NALA
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za
Mitaa (LAAC) imelipongeza Jiji la Dodoma kwa ukamilishaji wa barabara ya
kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 1.6 inayoelekea Hospitali ya Jiji na
kuufanya mradi huo kuwa wa kipekee ukilinganishwa na miradi iliyotekelezwa
katika maeneo mengine.
Akizungumza wakati wa ziara ya kamati hiyo ya kukagua miradi ya maendeleo Makamu Mwenyekiti wa LAAC, Abdallah Chikota, alisema kuwa kamati imeridhishwa na ubora wa utekelezaji wa mradi huo uliogharimu shilingi bilioni 2.8 kwa kutumia mapato ya ndani ya Jiji la Dodoma.
Alisema kuwa uwekaji wa miundombinu ya usalama ikiwamo
taa za barabarani ni hatua muhimu inayoongeza thamani ya mradi na kurahisisha
wananchi kufika Hospitali ya Jiji wakati wowote. Aidha, uwekaji wa taa, mitaro
na alama za barabarani umeboresha mpangilio na matumizi salama ya njia hiyo.
“Mradi umejengwa kwa kiwango ambacho tumeridhika. Pia,
tumeridhishwa na hatua ya kuwekwa kwa miundombinu ya taa za barabarani, ambazo
zimeboresha mwonekano wa eneo, usalama wa watumiaji wa barabara na mazingira
kwa ujumla, hasa wakati wa usiku. Tunalipongeza Jiji la Dodoma kwa utekelezaji
wa mradi huu,” alisema Chikota.
Kauli hiyo iliungwa mkono na mjumbe wa kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Kasuku Vijijini, Edibily Kazala alisema kuwa barabara hiyo imeonesha utofauti ukilinganisha na maeneo mengine ambayo kamati imefanya ziara ambapo hatua hiyo inastahili pongezi.
“Ujenzi wa barabara hii ya kilomita 1.6 kweli ni
tofauti kidogo na sehemu zingine tulizopita. Hapa wamefanya kazi nzuri sana,
wameweka taa, mazingira yamekaa vizuri na barabara yenyewe inaonekana kuwa na
ubora wa kuridhisha. Naomba niwape maua yao kweli,” alisema Kazala.
Akisoma taarifa ya mradi huo, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji
la Dodoma, Vincent Odero, alisema kuwa lengo kuu la mradi huo ni kurahisisha
wananchi kufika Hospitali ya Jiji kupata huduma za afya wakati wote ambapo
gharama ya mradi hadi kukamilika kwake ilifikia
shilingi bilioni 2.8.
Comments
Post a Comment